|  
 WAZIRI  wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amekoleza moto wa  sakata la kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans, akisema kamwe  hawezi kufungwa mdomo kupinga malipo ya Sh94 bilioni kwa kampuni  hiyo.Kauli ya Sitta imekuwa wakati kukiwa na taarifa kwamba waziri huyo  pamoja na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe wamebanwa na  Ikulu wakitakiwa wasizungumzie tena suala hilo.
 
 Hata hivyo,  akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana  Sitta alisema, "Naomba wananchi wafahamu, siwezi kufungwa mdomo kuhusu  kupinga malipo kwa kampuni ya kitapeli ya Dowans."
 
 Sitta ambaye  msimamo wake umeibua mjadala mzito nchini na hata ndani ya baraza la  mawaziri, alisema hajawahi kutishwa wala kufungwa mdomo kuhusu msimamo  wake.
 
 Kauli hiyo ya Sitta imekuja siku moja tangu gazeti moja la  kila siku kuripoti kwamba Rais Jakaya Kikwete amemfunga  mdomo, uamuzi uliodaiwa kufikiwa juzi katika kikao cha Baraza la  Mawaziri, kilichofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam.
 
 Habari hizo  zilidai kuwa Sitta na Dk Mwakyembe walikuwa na wakati mgumu kutetea  hoja ya kutaka Serikali isiilipe Dowans na kwamba hata Rais alisema  hafurahishwi na hukumu ya malipo hayo, hivyo kikao hicho kuwaamuru  mawaziri hao kutozungumzia tena suala hilo hadharani.
 
 Lakini jana  Sitta alisema: "Nitaendelea kupinga malipo ya Dowans. Sijawahi kuitwa  popote wala na mtu yeyote na kuambiwa nisizungumze suala hilo, hivyo  wananchi wasifikiri nimebadili msimamo".
 
 Aliongeza: "Taarifa  zinazosambaa ni za kupikwa tu, zisije zikawapotosha wananchi wakidhani  nimewasaliti katika hili, narudia tena sijafungwa mdomo."
 
 Mbunge  huyo wa Urambo Mashariki ambaye aliliongoza Bunge la Tisa katika vita  dhidi ya ufisadi, alifafanua kwamba si suala la Dowans tu bali  ataendelea kupinga mambo yote machafu kuhusu nchi.
 
 Aliweka bayana  kwamba nchi inahitaji viongozi wenye uwezo wa kusimamia vema maslahi ya  taifa bila hofu ili kulinda haki za wananchi na kuboresha maisha yao.
 
 Sitta  alinukuliwa akihoji kile kinachoitwa kukiuka dhana ya uwajibakaji wa  pamoja na kuweka bayana, kama dhana hiyo ingekuwa inaheshimika basi  uamuzi wa kuilipa au kutoilipa Dowans ungefanywa kwa pamoja.
 
 Alisema  haiwezekani dhana ya uwajibikaji wa pamoja ifanyike bila kushirikisha  wengine halafu mwisho itolewe taarifa ya uwajibakaji wa pamoja.
 
 "Halafu  kuna watu wanazungumzia nimekiuka dhana ya uwajibikaji wa pamoja,  uwajibikaji wa pamoja ni lazima uamuzi ushirikishe wengine si mmoja  kuamua halafu ifahamike ni uwajibakaji wa pamoja," aliongeza.
 
 Sitta  pia amekuwa akihoji kasi ya malipo hayo kwa kampuni ya Dowans wakati  nchi ina madeni mengine kama ya Benki ya Dunia na IMF, lakini bado  hayajalipwa kwa kasi kama hiyo.
 
 "Lakini, hii haraka ya kuilipa  Dowans ni ya nini?  Nchi hii ina madeni ya muda mrefu kama yale ya Benki  ya Dunia na IMF, lakini hakuna uharaka wa kulipa kama huu sasa kasi hii  inatoka wapi?" alihoji.
 
 Alisema nchi ina matatizo mengi ikiwemo  ya kiuchumi, hivyo haingii akilini kuona Watanzania wanalipa kiasi  hicho kikubwa cha fedha kwa kampuni ya kitapeli.
 
 Tayari msimamo  wa Sitta ulimfanya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias  Chikawe, kutoa vitisho kwa mawaziri wenzake akiwataka wakae kimya na  kuacha kuzungumzia sakata hilo vinginevyo wajiondoe kwenye Serikali.
 
 Hata  hivyo, wakosoaji wamemwelezea Chikawe kama ambaye pia amekiuka taratibu  kutokana na kuzungumza suala hilo kwenye vyombo vya habari, badala ya  taratibu za kiserikali.
 
 Tangu Mahakama ya Usuluhishi ya Biashara  ya kimataifa (ICC Court) kutoa hukumu ya mwezi Novemba, ikitaka Tanesco  ilipe Dowans, Sitta alikuwa waziri wa kwanza kupinga malipo hayo  hadharani.
 
 Hata hivyo, pamoja na Sitta kupinga, Mwanasheria Mkuu  wa Serikali, Jaji Fredrick Werema alikwisha kusema bayana kwamba  Serikali haiwezi kukata rufani katika sakata hilo, lazima ilipe faini  hiyo.
 
 | 
3 comments:
we need such kind of people in TZ..
tukiwa nao km 10 hv tutasogea sn
Ndio watanzania wenye uzalendo tuliobakia nao! Na mimi namkubali sana Mheshimiwa!- Chriss - Sinza
TZ viongozi wote wangekuwa kama SITTA nchi ingekuwa mbali sana,neno ufisadi tungekuwa tunalisikia tuu!! Mungu ampe nguvu aendelee kulitetea taifa letu na watu wake
Post a Comment