Tuesday, December 21, 2010

IVI NI KWELI TUMESHINDWA KUMSAIDIA DADA YETU HUYU MSOMI ALIYEPATA 'AJALI' YA AKILI...


Jane Sosovele


YUMKINI wengi wanaomuona Jane Sosovele katika maeneo ya Posta Mpya na mengine ya jirani hudhani kwamba ugonjwa wake wa akili alionao haukumpa fursa ya kujua kusoma na kuandika.

Wanapomuaona akiongea maneno yasiyokuwa na mbele wala nyuma, akiwa amebeba mfuko wa plastiki ambao ndani yake huwa na makaratasi ya kuokoteza, huku akiomba chochote kwa wapita njia huamini kwamba hana analolijua.

Hao wamekosea. Mwanamke huyu ni msomi aliyekuwa tegemeo kubwa katika fani ya mawasiliano ya simu katika Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).

"Jane Sosovele alikuwa mtumishi wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu Tanzania kuanzia Julai 31, 1987 katika nafasi ya 'Telecomms Controller' baada ya kuhitimu Shahada ya Bsc General ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam... Kufuatia kugawanywa kwa Shirika la Posta na Simu Tanzania na kuundwa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na Shirika la Posta Tanzania (TPC) mwaka 1994, aliendelea na utumishi katika kampuni ya Simu Tanzania hadi Julai, Mosi 1998 alipostaafishwa kwa sababu za kiafya," anasema Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu wa TTCL, Juvenal Utafu.

Pengine hiyo ndiyo sababu ya Jane kupendelea kukaa maeneo ya hayo ya Posta Mpya kwani ni sehemu inayomrejeshea kumbukumbu njema za maisha yake ya zamani ambayo kuyapata tena ni kudra za Mungu.

Hata unapobahatika kukaa naye utagundua kuwa ni msomi 'aliyepata ajali' kwani mbali ya kutumia misamiati mingi ya Kiingereza, anazungumzia mambo kadha wa kadha ya kimataifa hata kama ni katika njia ambazo hazieleweki vyema. Kwa mfano, mara kwa mara hupendelea kusema wakuu wa posta wapo katika mkutano mkuu Geneva (Uswisi), safari yake ya Lebanon imekaribia, magari yake yamepotea bandarini au akisema, anatunza risiti ili akalipwe pesa za vikao.

Ni vigumu kufanya naye mahojiano kwani anachanganya mambo. Lakini nilibahatika kuzungumza naye na alinieleza yafuatayo:
“Ni vigumu kutatua tatizo ambalo limejitokeza kwa muda mfupi kwani mabadiliko ya mume wangu yalikuwa ya ghafla mno,” anasema na ghafla anachanganya habari za risiti.

Anaendelea: “Nilipokuwa Ujerumani nilinunua magari matatu, makochi na friji lakini sijui vilipotelea wapi, wanasema vimeibiwa bandarini, nilikuja na zawadi nyingi za watoto sijui kama walizichukua!”

Mmoja wa watu wanaomfahamu kwa karibu mwanamke huyo anasema: “Huwezi kuamini, Jane ambaye wengi humpita hapa na kumdharau wakiwa hawana habari naye, kabla ya kuvurugika akili alikuwa ni Injinia.”

Anasema kama si kupata matatizo hayo ya akili Jane angekuwa miongoni mwa watu wenye nyadhifa mkubwa katika tasnia ya sayansi kwa sababu anasema alikuwa mwerevu na mchapakazi hodari na makini kwelikweli.

Kuna simulizi nyingi zinazotolewa juu ya ni sababu gani iliyomfikisha mwanamke huyo katika hali hiyo. Inayotajwa zaidi ni mtikisiko wa ndoa yake mnamo mwaka 1997.

“Jane ni msomi huyu! Usimuone hivi. Ameshatembelea nchi nyingi tu duniani lakini mapenzi ndiyo yaliyomfanya awe hivi, mume wake ambaye ni Profesa wa hapo Mlimani ndiye aliyemsababishia matatizo hayo,” anadai mwanamke mmoja ambaye alikuwa akifanya naye kazi bila kutaka kutaja jina lake na kuongeza:

"Inasikitisha kuona mtu ambaye angekuwa na maisha mazuri lakini sasa hivi ana ombaomba, akiwa hajui familia yake iko wapi na wala hajielewi! Lakini yote hayo yamesababishwa na mapenzi ambayo yamekuwa yakitajwa kila siku kuwa ni sumu."

Ndugu wa Jane aliyejitambulisha kwa jina la Mama Mariamu, anasema mama huyo wa watoto wawili akiwa Chuo Kikuu, mwaka 1984 alibeba ujauzito wa mtoto wake wa kwanza Daudi kabla ya kufunga ndoa mwaka 1986. Mwaka mmoja baadaye aliamua kumfuata mumewe Ujerumani pamoja na kusoma.

Safari yake ya Ujerumani ilimgharimu kwani kwa mujibu wa taarifa ya Utafu, aliomba likizo ya bila malipo ambayo ilikataliwa na mwenyewe kuamua kuondoka bila kibali hivyo kufutwa kazi Januari, 1988.

"Aliomba likizo bila malipo baada ya miezi mitatu tu ya ajira kwa ajili ya kwenda Ujerumani kuishi na mumewe ambaye alipata nafasi ya kusoma katika iliyokuwa Jamhuri ya Ujerumani Magharibi hapo mwaka 1987 hadi 1988 lakini likizo hiyo ilikataliwa kwa sababu kanuni za utumishi hazikuruhusu likizo bila malipo kwa mtumishi aliyekuwa bado kwenye kipindi cha majaribio."

Mama Mariamu anasema wakati ndugu yake huyo akiwa safarini Ujerumani alikuwa na ujauzito wa mtoto wake wa pili, Ibrahim na matatizo ya ndoa yalianzia huko kwani aliporudi hakuwa na amani tena.

Baada ya kurejea, Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu wa TTCL, anasema Jane aliomba tena kuendelea na kazi... "Aliajiriwa upya kuanzia Januari 23, 1989 kwa vile sifa yake kielimu ilikuwa inahitajika ndani ya shirika."

Hata hivyo, Utafu anasema: "Tabia yake ilianza kubadilika na kuwa isiyokuwa ya kawaida kwa kile alichodai kwamba ana matatizo yake binafsi ya kifamilia na alionyesha wazi kwamba amechanganyikiwa. Hatua zilichukuliwa na alipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Muhimbili wakati huo kwa muda mrefu bila mafanikio. Kwa ushauri wa jopo la madaktari, alistaafishwa kazi kwa ajili ya ugonjwa Julai Mosi, 1998."

Kwa upande wake, Mama Mariamu anadai kuwa baada ya kuona mke wake amechanganyikiwa, mumewe alimrudisha kwa dada yake Mabibo ambako ndipo alipomuolea.

“Tulishangazwa na kitendo cha Sosovele kumrudisha mama Ibrahim (Jane) akiwa amechanganyikiwa tena bila kufafanua chochote na wala kufuatilia afya ya mke wake na mpaka leo amekuwa hana ukaribu kabisa na sisi hatuna mawasiliano naye hiyo inatuhakikishia kuwa yeye ndiyo chanzo cha yote,” anasema.

Anasema anafahamu kwamba mume huyo yupo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lakini hajui anakoishi na watoto wa ndugu yake.

Akizungumzia madai hayo, mume wa Jane, Profesa Hussein Sosovele anasema: “Mimi na Jane tumeachana muda mrefu. Mambo yake na yangu yaliisha miaka zaidi ya 10 iliyopita kwa hiyo habari zake sizijui.”

Profesa Sosovele anakiri kwamba yeye na Jane walipitia matatizo ya ndoa na akamrudisha kwa wazazi wake, tofauti na madai ya Mama Mariamu, profesa huyo anadai kwamba wakati wanaachana mtalaka wake alikuwa hana tatizo lolote la akili.

Anasema hata alipopata taarifa juu ya matatizo yaliyomsibu, alijaribu kumsaidia lakini hakupata ushirikiano kutoka kwa ndugu zake.

1 comment:

Anonymous said...

hey Ben
daa nimesoma habari hii kwa uchungu sana inasikitisha sana
kweli hujafa hujaumbika
n ways hakuna linalotokea bila sain ya mwenyezi mungu yeye ndo mjuaji wa ya jana leo na kesho
asante kwa hii posti mungu atuongoze ktk shughuli zetu za kila siku inshala

Website counter