Monday, October 11, 2010

SHIME SHIME SERIKALI MSAIDIENI MTOTO HUYU MWENYE KIPAJI CHA AJABU...

Farida: Mtoto mwenye kipaji cha ajabu kukariri lugha za kigeni Send to a friend


Farida Fowadi

Zulfa Mfinanga

SIO jambo la kawaida hasa Tanzania kumwona mtoto mdogo mwenye umri wa miaka minne au sita akizungumza kwa usafaha, lugha mbalimbali za kigeni ikiwamo Kiingereza, Kifaransa au Kijapan wakati hajawahi kuishi nje ya nchi au kusoma shule za mchepuo wa lugha hizo.

Watoto wengi wanaosoma katika shule za kawaida maarufu kama za kina Kayumba hususan zile za vijijini, wanafunzi huanza kujua kuzungumza Kiingereza wakiwa darasa la saba na wengi humaliza bila hata kujua kutamka neno lolote kwa ufasaha.

Kutokana na wanafunzi wengi wanaosoma katika shule hizo kutokuwa na maendeleo mazuri ndio maana wazazi wenye uwezo wamekuwa wakiwasomesha watoto wao katika shule za kimataifa ambako hufundishwa masomo yote kwa lugha ya Kiingereza na pengine Kifaransa.

Ni jambo la kawaida kabisa ukienda katika shule ya kimataifa kusikia wanafunzi wakizungumza Kiingereza au Kifarasa, lakini sio jambo la kawaida kusikia wanafunzi wa shule za msingi za kina Kayumba, wakizungumza lugha hiyo muda wote wanapokuwa shuleni.

Lakini Farida Fowadi (9) anayesoma darasa la tatu Shule ya serikali ya Msingi Ndala A iliyopo Manispaa ya Shinyanga, ameonekana kuwa tofauti na watoto wengine wa shule za msingi za kawaida baada ya kuonyesha kipaji cha ajabu katika kuzungumza lugha mbalimbali za kigeni tena bila kufundishwa na mtu yeyote.

Mwanafunzi huyo ana kipaji cha kukariri hotuba mbalimbali zinazotolewa kwa lugha yoyote inayozungumzwa duniani na baadaye kutamka kwa ufasaha kila neno, jambo ambalo linamfanya aonekana wa ajabu shuleni na eneo analoishi.

Kipaji hicho kinafanya baadhi ya watoto wenzake kumwita zimwi wakimaanisha kutokuwa mtu wa kawaida katika jamii ya binadamu.

Farida ambaye ni mtoto wa pili katika famili ya watoto wanne waliotoka kwenye tumbo la Jannat Fowadi mkazi wa Mtaa wa Ndala uliopo Manispaa ya Shinyanga, kimsingi hazijui lugha hizo, lakini anaweza kuzikariri na kutamka neno moja baada ya lingine kwa ufasaha kabisa.

Kipaji cha Farida kilianza kujionyesha tangu akiwa mtoto mdogo na watu walianza kumfahamu zaidi mwaka 2008 kipindi ambacho alikuwa na umri wa miaka sita.

Alianza kufahamika baada ya kutoa hotuba katika sherehe za Serikali za Mitaa (Tamisemi) zilizofanyika kitaifa mkoani Shinyanga.

Mama yake Jannat anasema ingawa alijua kuwa mtoto wake ana kipaji cha kukariri vitu na kuvitunza bila kusahau, alimshangaa siku hiyo, alipoweza kukariri hotuba ndefu aliyoitoa kwa lugha ya Kiingereza.

Katika sherehe hizo mtoto huyo alikuwa ni miongoni mwa watu waliomkaribisha mgeni rasmi ambaye alikuwa Waziri wa Tawala za mikoa na serikali za mitaa, Celina Kombani ambapo alimkaribisha kwa lugha ya Kiingereza na mwisho kuimba wimbo wa Kiingereza alioimba kwa mtindo wa Rap.

Jannat anasema hata yeye anashangaa kuona mwanaye akizungumza kiingereza au lugha nyingne za kigeni kwa vile anaamini haitokani na kufundishwa darasani.

Anasema mwanaye anasoma shule za kawaida za mitaani ambazo zinafundishwa masomo ya awali kwa lugha ya kiswahili.

"Mtoto huyu anakipaji kikubwa cha kukariri na kuzungumza bila kukosea hata neno moja," anaeleza Jannat.

Kwa mujibu wa Jannat baada ya watu wengi mjini Shinyanga kugundua kipaji cha mtoto huyo, wamekuwa wakimchukua kwenda kutoa hotuba kwa lugha za Kiswahili, Kiingereza au Kifaransa katika sherehe zao na kumpatia kiasi kidogo cha fedha.

Anakiri kuwa hali hiyo imemfanya asiende shule mara kwa mara hasa inapotokea sherehe hiyo ikaangukia katika siku ya shule.

"Huwa nakwenda kuomba ruksa shuleni ili mwanangu aende alikoalikwa. Hii inatusaidia kupata fedha za kujikumu," anasema na kuongeza kuwa hali yake ya maisha sio nzuri.

Jannat alisema analazimika kwenda na mwanaye huyo maeneo yote anayoalikwa kwa ajili ya kuangali usalama wake.

Imefikia wakati ukifika Shinyanga Mjini na kumwulizia mtoto huyo mwenye kipaji cha kuzungumza lugha za kigeni yeyote anayeishi huko anaweza kukuelekeza kutokana na umaafuru aliojizolea mtoto huyo.

Hivi sasa ni nadra kumkosa Farida katika matamasha mbalimbali hususani yanayohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na siasa mkoani hapa.

Mratibu wa shughuli mbalimbali Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga, Said Bwanga alikiri kumtumia mtoto huyo katika matamasha mbalimbali kutokana na kipaji chake.

Bwanga anamwelezea Farida kuwa ni mwepesi sana kukariri lugha za kiingereza na kifaransa ingawa hazijui kabisa.

“Kwa kweli ukimsikia unaweza kuamini kuwa mtoto huyo amezaliwa Marekani au Ufaransa. ukimsikia huwezi kuamini kama amekariri, hata ukimwandikia kitabu kizima kwake haina tabu. Utashangaa siku hiyo, na wala hasomi yeye ni kukariri tu,” alisema Bwanga.

Farida mwenyewe anakiri kuwa anajua kuwa ana uwezo mkubwa sana wa kukariri lugha hizo na kutamka kwa ufasaha, lakini hajui maana ya maneno hayo.

Anasema kipaji chake hakitokani na kufundishwa darasani kwani shuleni anajifunzi Kiingereza lakini haelewi na kwamba Kifaransa ndio kabisa hakifundishwi.

Hata hivyo, mbali na kujivunia kipaji hicho Farida anasema anahuzunika na kufadhaika wenzake wanavyomwita zimwi kwa sababu ya kipaji hicho.


"Hali hiyo inanifanya nijione mnyonge na kufedheheka sana," alisema.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Ndala A anayosoma Farida, Justina Ndimila anasema kuwa maendeleo ya Farida darasani si mazuri sana na anashangaa kusikia ana kipaji cha kukariri na kuzungumza lugha za kigeni kwa ufasaha.

"Mtoto huyo hana mahudhurio mazuri darasani, na kitendo hicho kinamfanya awe na maendeleo duni," alisema


Hata hivyo, mwalimu huyo alieleza kuwa baada ya kufuatilia ili kujua sababu ya utoro wake waligundua kuwa mtoto huyo haendi shule kutokana na kutumika katika matamasha.

Anakiri kuwa mbali ya kuwepo tatizo hilo, uongozi wa shule haujawahi kumwita mzazi wake na kuzungumza naye kuhusu kipaji hicho cha mwanaye.

Mwalimu wa somo la Kiingereza katika darasa la tatu, Grace Mrefu, anasema maendeleo ya Farida katika somo hilo, si mazuri.

Grace alisema waliposikia kuwa Farida ana kipaji hicho yeye pamoja na walimu wenzake walimwita na kumwambia azungumze hotuba alizowahi kuzitoa jukwaani kwa lugha ya kiingereza, alirudia na kuzitamka kwa usafaha bila ya kukosea.

Mwalimu Mrefu alisema hata wao walishangaa kusikia mtoto huyo anavyozungumza vizuri tena kwa ufasaha lugha hiyo ambayo hata hivyo darasani inamshinda.

Kutokana na umahiri huu wa Farida kuzungumza lugha hiyo, CCM Mkoa hivi karibuni ilimwandaa kuzungumza mbele ya mgombea urais wa chama hicho, Jakaya Kikwete wakati wa kampeni zake mkoani humo.

Hata hivyo alishindwa kufanya hivyo baada ya mgombea huyo kukosa muda kutokana na ratiba yake kubana.

Kufuatia hali hiyo uongozi wa shule hiyo umesema utafanya jitihada za kukaa na wazazi wa mtoto huyo ili kujua kwa undani kipaji chake huku mama mzazi wa Farida akiwaomba wafadhili kujitokeza ili kuweza kumsaidia zaidi kielimu.

Jannat anasema angependa kuona Farida anasoma katika shule za watoto wenye vipaji maalumu ili aweze kukiendeleza kipaji chake, hivyo anawaomba wasamaria wema kujitokeza kumsaidia ili aweze kuendelezwa kipaji chake.

No comments:

Website counter