|  
  Kiungo  wa Simba Rashidi Gumbo akaipiga hesabu za kumtoka beki wa JKT Ruvu,  Stanley Nkombo wakati wa mechi ya ligi kuu iliyofanyika kwenye uwanja wa  Jamuhuri mjini Morogoro, Simba ilishinda 2-1MABINGWA  watetezi Simba wamerejea kileleni mwa Ligi Kuu baada ya kupata ushindi  wa pili mfululizo tangu walipofungwa na mahasimu wao Yanga waliopoteza  dira kwa suluhu nyingine jana.
 
 Simba wailishuka kwenye uwanja wa  Jamhuri kuwakabaili maafande wa JKT Ruvu na kuwachakaza kwa mabao  2-1  ikiwa na siku tatu tangu ilipoicha AFC Arusha 3-1 na kukalia kiti cha  uongozi wa ligi kwa tofauti ya mabao ya kufunga mbele ya Yanga  iliyolazimishwa suluhu ya pili na Azam kwenye uwanja wa Mkwakwani jijini  Tanga.
 
 Kiungo Rashidi Gumbo alikuwa wa kwanza kufunga bao kwa  Simba  dakika 25, kwa shuti na kumshinda kipa wa JKT Ruvu, Shaibu Issa,  kabla ya mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi kuifungia  Simba bao la pili dakika 43, baada ya kumlamba chenga beki Stanley  Nkomolo na kupachika mpira huo wavun.
 Gumbo alipoteza nafasi ya kufunga bao lake pili pale alipopaisha juu kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Hillay Echesa.
 Maafande  wa JKT walirudi kipindi cha pili wakiwa makini zaidi kwa kuongeza  ulinzi golini kwao na kufanya mashambulizi machache ya kushitukiza.
 
 Mshambuliaji  chipukizi Hussen Bunu aliifungia JKT bao la kufutia machozi zikiwa  zimebakia dakika 9, mpira kumalizika kwa kichwa akiunganisha pasi ya juu  ya nduguye Abdalah Bunu kufanya matokeo kuwa 2-1.
 
 Katika mchezo  huo Simba iliwatoa Partick Ochan na Amri Kiemba na kuwaingiza Mussa  Mgosi na Abdalhaman Humoud wakati JKT wao ilimpumzisha  Hussein Kikutwa  na kumwingiza Pius Kisambale mabadiliko yalikuwa ni faida kubwa maafande  hao walipofanikiwa kupata bao la kufutia machozi dakika 81.
 
 Kocha wa Simba, Partick Phiri alisema amefurahisha na matokeo hayo na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake.
 
 Jijini  Tanga, Yanga ambayo tangu ilipoifunga Simba Oktoba 16, imezungukwa na  wingu la tetesi ya kocha wao Kostadic Papic kutaka kuondoka kwa sababu  ya kudai malipo ya mishahara yake, jana alishudia vijana wake  wakilazimishwa sare ya tatu msimu huu.
 
 Azam walianza mchezo kwa  kasi katika dakika 10 za mwanzo walifanikiwa kufika lango kwa Yanga mara  tatu, huku kiungo wake Ramadhani Chombo 'Redondo' akikosa bao la wazi  kwa kushindwa kumalizia pasi ya Suleiman Kassim dakika 9.
 
 Yanga  walifanikiwa kufika langoni kwa Azam kwa mara ya kwanza dakika ya 16,  kwa mpira wa adhabu uliopigwa na Athumani Idd 'Chuji',
 kama  ilivyokuwa kwenye mchezo dhidi ya Simba viungo wa vijana hao wa Kostadic  Papic waliendeleza mtindo wao wa kutembeza viatu katikati ya uwanja  hali iliyosababisha Chuji na Godfrey Bonny kuzawadi kadi za njano dakika  13 na 14 kutoka kwa mwamuzi Allanus Luwena wa Mwanza.
 
 Winga  Mrisho Ngasa aliwachambua mabeki wa Yanga na kupiga pasi nzuri kwa John  Boko aliyepiga shuti lililotoka nje uwanja, naye kinara wa ufungaji  msimu huu Jerryson Tegete alipoteza nafasi ya wazi ya kufunga baada ya  kupokea pasi nzuri kutoka kwa Nurdin Bakari, lakini shuti lake liliishia  mikono mwa kipa wa Azam, Vladimir Niyonkuru.
 
 Dakika moja kabla  ya mapumziko Kassimu alikosa bao baada ya kipa Yaw Berkyo kufanya  uzembe, lakini beki ya Yanga chini ya Nadir Haruob ilikuwa makini  kuondoa hatari hiyo.
 
 Mashabiki wa Yanga waliofurika uwanjani hapo  walimvamia mwamuzi Luwena wakitaka kumpiga, lakini askari wa usalama  waliweza kuwahi na kuingilia kati na kuwasindikiza kwenye vyumba vya  kubadilishia nguo.
 
 Kutokana na kuendekezwa kwa imani za  kishirikina katika soka ya Tanzania, wachezaji wa Azam waligoma kuingia  vyumbani kwenye Uwanja wa Mkwakwani na kupewa mawaidha yao uwanjani.
 
 Kipindi  cha pili kilianza kwa kasi huku Yanga wakionekana kutafuta bao la  kuwaweka vizuri kileleni, lakini wachezaji wake Chuji, Nsa na Tegete  walipoteza nafasi za kufunga dakika ya 46, 54 na 58 na kuwaacha  mashabiki wao wakishika vichwa.
 
 Beki wa Azam, Erasto Nyoni  alitaka kumzawadi Tegete bao dakika ya 76, baada ya kurudisha mpira  kichwa kwa kipa wake Niyonkuru wakati Jerry akiwa katikati yao, lakini  kipa huyo aliyefanya kazi ya ziada kuudaka mpira huo.
 
 Papic  alisema mwisho wa mchezo timu yake haikucheza vizuri katika kipindi cha  kwanza, lakini walibadilika dakika 45 za mwisho ila bahati haikuwa yao  kwani washambuliaji wake walipoteza nafasi nyingi za kufunga.
 
 Naye  Itamar alisema amefurahishwa na matokeo japokuwa wachezaji wake  walizidiwa ujanja kipindi cha pili hivyo kuwafanya viungo kupoteza uwezo  wao wa kuwachezesha washambuliaji wake.
 
 | 
No comments:
Post a Comment