Monday, September 12, 2011

LEO KWENYE KONA YA MAHABA...


Kwa mara nyingine tena tunakutana kwenye safu yetu hii ya MAHABA!

Rafiki, wanawake wengi hulia na kujutia kuwepo katika ndoa, hii ni kutokana na kuhisi au kujua kuwepo kwa usaliti kwa waume zao. Ukweli ni kwamba suala la kusalitiwa linaumiza sana, hakuna atakayekuwa tayari kukubali usaliti katika penzi lake.

Huo ndiyo ukweli, lakini pamoja na ukweli huo umewahi kujiuliza kwa nini mpenzi wako anakusaliti? Umewahi kufikiri kwamba hata wewe unaweza kuwa chanzo cha mpenzi wako kukusaliti?

Kama hujawahi kufikiri basi fahamu kwamba kama usipokuwa makini katika maeneo fulani katika ndoa yako, unaweza kuwa chanzo cha mumeo kukusaliti. Vipengele vifuatavyo, vinafafanua hilo kwa undani zaidi:

UNATAMBUA MAJUKUMU YAKO?
Hili linawashinda wengi katika maisha ya ndoa na waume zao kwa kukosa kujitambua kuwa yeye ni nani na wajibu wake katika ndoa yake ni upi. Hapo awali kabla ya kuingia katika ndoa na mumeo ulikuwa ukimnyenyekea na kujitahidi kadiri ya uwezo wako kumwonyesha mapenzi motomoto lakini sasa baada ya kuingia katika ndoa umebadilika.

Ulikuwa msafi mwenye kumjali wakati wote na kumwonyesha kuwa yeye ni muhimu maishani mwako na wewe ni muhimu sana katika maisha yake. Kuwa naye karibu wakati wote na kumshauri hasa akiwa katika matatizo na sononeko la moyo au msongo wa mawazo vilimvutia na kuona thamani yako kwenye maisha yake.

Huenda hapo awali ulikuwa mshauri wake mkubwa wa mambo mbalimbali ya kikazi na wakati mwingine mambo yake binafsi, wakati alipokuwa na majaribu ya kufukuzwa kazi au kupata balaa la madeni kazini kutokana na uharibifu au upotevu wa mali ya anapofanyia kazi kwa kumshauri au hata kumsaidia kifedha.

Sababu hizo na zingine nyingi ulizokuwa ukimfanyia wakati mkiwa wachumba huenda ndizo zilizomsukuma akusogeze karibu ili aishi na wewe kwa kutambua umuhimu wako katika maisha yake lakini sasa umebadilika!

Mwanaume anahitaji mwanamke wa kumshauri na kumpa moyo hasa anapokuwa kwenye majaribu na matatizo mbalimbali ya kimaisha.

Kama awali ulikuwa ukimfanyia hivyo mumeo na sasa umeacha ni wazi kwamba atakapokuwa na msongo wa mawazo au matatizo flani atakwenda baa ambako atakutana na mwanamke wa nje na akithubutu kumweleza yaliyomsibu atapata tulizo kwa sababu wanawake wa nje ni mahodari wa kufariji waume za watu.

Baadhi ya wanawake wakishaingia katika ndoa, hujisahau na kuona kuwa wao ni wao na kama walichotaka wameshakipata hivyo kujisahau na kutowapa wapenzi wao mapenzi motomoto. Kikubwa unachopaswa kutambua wewe mwanamke ni kwamba wanaume wanapenda kuona wake zao wanakuwa kwa ajili yao na kuwafanyia vituko vya mahaba kila wakati.

Kadhalika hupenda kuona wake zao wanakuwa karibu nao wanapokabiliwa na matatizo mbalimbali ya kimaisha. Hakika utakaposhidwa kumjali mumeo huona ni afadhali atafute kitulizo kingine ambapo hata hivyo mara nyingi hukimbilia baa kutafuta kitulizo cha msongo wa mawazo.

Wengine hushinda kutwa nzima nyumbani wakihudumia mifugo au wakifanya shughuli ndogondogo za kila siku kama kufua, kupiga deki na kazi nyingine za mama wa nyumbani baada ya hapo hubaki na nguo alizoshinda nazo kutwa nzima hadi mumewe anaporejea kazini humkuta akiwa na nguo hizo chafu huku akinuka jasho ambapo kwa kiasi kikubwa linamkera mume atakaporudi kutoka kwenye mihangaiko yake.

Hivi unafikiri kwa misingi hiyo mumeo ataacha kutoka nje ya ndoa kweli? Kama unakuwa mchafu wakati wote, humfurahishi, huvutii kama zamani unadhani atafanya nini kama siyo kukusaliti?

Lazima utambue majukumu yako katika ndoa yako. Majukumu yako hayaishii kumfulia, kumpasia na kufanya usafi nyumbani pekee! Majukumu yako ni pamoja na kuhakikisha mumeo anafurahia penzi lako pamoja na kumsaidia katika matatizo mengine ya kikazi na kiakili. Anza kubadilika sasa kabla hujampoteza mumeo.

1 comment:

Anonymous said...

MMH MBONA MUME MUME TUU! NA MUME KWA MKEWE JE? WANAWAKE TUNATAKA HASWA RAHA, UNALIKUTA JIANAUME LINGINE LINALALA TU, HALIJUI KUMPA MAHABA MKEWE ANAONA AKISHA MALIZA YEYE BASI... RUDINI JANDO.. SIO KUSEMA WANAWAKE TU

Website counter