Sunday, August 21, 2011

HESHIMA YA HAYATI LUTENI GENERAL MAYUNGA , LAKINI MALIPO 'DUNI'...


Marehemu Luteni General SILAS MAYUNGA 'kulia' akiwa na General DAVID MUSUGURI alie kushoto! Picha hii ilipigwa kipindi walipowasili nchini kutoka Vitani kumsambaratisha 'Nduli' IDDI AMIN DADA wa UGANDA!
KWA kuwa sala husaidia, ni bora nikamuombea pepo ya heri kwa mwenyezi Mungu ili Luteni Jenerali Silas Mayunga ‘Mti Mkavu’ apumzike kwa amani baada ya utumishi wake uliotukuka kwa taifa hili.

Kazi ya Mungu haina makosa. Hili naliamini na wala sipingani na Muumba kuhusu kuwepo kwa kanuni ya siku ya kuzaliwa na ya kufa. Ndiyo maana nimepokea kifo cha shujaa huyo kwa mikono miwili, ila nikitafakari mchango wa heshima wa Mti Mkavu kwa Watanzania nabaini kasoro.

Sote tunafahamu Jenerali Mayunga enzi zake aliweka rehani uhai wake, akatanguliza uzalendo kwa taifa lake, akawa tayari kusimamia oparesheni ngumu zaidi ya kijeshi iliyopewa jina la Chakaza ili kumng’oa nduli Idd Amin wa Uganda aliyewatusi Watanzania na kutaka kudhulumu ardhi yao mwaka 1979.

Nawaza, mtu kama huyu ambaye licha ya kuwa mtumishi mtiifu jeshini na amepata kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro, Balozi wa Tanzania nchini Nigeria na Jamhuri ya Kongo, amekufa katika hali gani?

Kumbukumbu zinaonyesha kwamba mpaka Mti Mkavu anapelekwa nchini India kwa matibabu, mzee huyu alikuwa akiishi maisha ya dhiki sana ambayo kusema kweli ukilinganisha na mchango wake kwa taifa, haulingani hata kidogo.

Watu wenye huruma kama mimi wanaweza kujiuliza, kosa la Jenerali Mayunga kwenye serikali hii lilikuwa ni nini? Je, ni kutumikia taifa kwa uaminifu na moyo wa uzalendo ndiyo dhambi iliyomfanya amalizie vibaya maisha yake au alizubaa kuhujumu mali za umma ndiyo maana alipuuzwa?

Fikra nyepesi zinaonyesha kuwa, serikali imekosa shukrani kwa mashujaa wake, ikitafutwa tafsiri nyingi itakuwa ni kuichosha akili kwa vitu vilivyokuwa wazi. Mti Mkavu hakupewa shukrani kwa mchango wake, inatosha kusema hivyo.

Moja kati ya mifumo mibaya iliyojengwa kwenye nchi hii ni ya kutothamini michango ya kizalendo wa Watanzania kwa ngazi zote, maana ukiachilia mbali Mti Mkavu ambaye amefariki dunia akiwa mwaminifu, kuna wastaafu wengine wameachwa wakiteseka bila msaada wala heshima yo yote.

Hivi karibuni tumewasikia baadhi ya wanajeshi na watumishi wengine wa umma wakilalamika kupata mafao hafifu, mmoja wapo ni mkuu wa zamani Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Mirisho Sarakikya ambaye alisema pensheni ya shilingi 50,000 wanayopewa haitoshi kuendesha maisha.

Inawezekana kwa tafsiri za juujuu mtu asione hasara ya kuwepo kasumba hii mbaya ya kuwatelekeza watu waliotetea taifa na kujitolea utu wao kwa manufaa ya jamii kama wafanyavyo viongozi wa nchi hii, lakini ukweli unabaki kwamba tabia hii inaua moyo wa uzalendo kwa Watanzania.

Somo la utumishi uliotukuka na uamanifu wa mali za umma ambalo serikali inatamani liwaingie Watanzania haliwezi kueleweka kwa vijana wanaoingia jeshini leo huku wakiambiwa au kumuona mkuu wa majeshi wa zamani akikata mitaa na kandambili miguuni.

Wimbi la ufisadi na uhujumu uchumi linalotikisa nchi yetu sasa hivi linatokana na wananchi kushindwa kufahamu faida za uaminifu ni zipi, ikiwa akina Mti Mkavu walioweka heshima ya nchi wameachwa katika hali duni mpaka wanakufa.

Taswira ya Watanzania wengi imewafikisha mahali pa kuamini kwamba nafasi za uongozi na vyeo kama si utumishi wa umma kwa ujumla wake zinaweza kuwa na maana kwao kama watajitajirisha mapema kwa wizi kuliko kusubiri bila mafanikio kuheshimiwa na serikali.

Kwenye nchi hii mafisadi wana heshima kubwa kuliko wazalendo wa kweli. Utajiri usiokuwa na vyanzo una ramani ya utukufu machoni pa watu, kuliko umasikini unaolinda rasilimali za taifa. Jambo hili ni la ajabu sana.

Ukipata fursa ya kufuatilia mifumo ya nchi nyingine zinazoheshimu zana ya uzalendo utabaini kuwa, heshima haiendi kwa watu wasiofuata misingi na sheria za nchi. Ndiyo maana ukienda Marekani kwa mfano, waliokuwa wafungwa wa Vita ya Pili ya Dunia wanavaa beji maalumu za utambulisho zenye nembo ya POW (Prisoners Of War).

Beji hizo za POW zinawawezesha watu hao kujulikana na jamii imekuwa ikiwapa heshima.
Kwa Tanzania, tumeshindwa nini kutambua mchango wa mashujaa wetu na kuwapa beji zitakazowafanya waheshimike kwa kupewa kipaumbele wanapokwenda kwenye foleni za kununua Luku za umeme au hata kwenye zamu za kuingia kumuona daktari, ili waone fahari ya kuwa waaminifu kwa taifa?

Natoa mwito kwa serikali na hasa kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ahakikishe kwamba mashujaa wetu, nikimaasha watu wote wanaotoa michango mizuri inayoliletea heshima taifa, wanathaminiwa na si kupuuzwa.
Nashindwa kusema mengi, ila KALALE PEMA JENERALI MTI MKAVU, nitaenzi uzalendo wako!

No comments:

Website counter