Wednesday, August 31, 2011

JAMANI WAZAZI KUWENI MAKINI NA HAYA 'MABASI YA SHULE' KWA WATOTO WENU OHOOO...UZOEFU wangu mdogo kama mtoto wa mjini unaonyesha kwamba wazazi wengi wako makini kulipa ada, lakini sio kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni.Sio ufuatiliaji wa maendeleo ya taaluma tu, tangu kuanza kwa utaratibu wa mabasi ya shule, wazazi hao hao wamekuwa wakilipa gharama za nauli kwa watoto wao pasina kufuatilia ubora na hata usalama wa vyombo husika.

Uchunguzi wangu wa hivi karibuni umebaini magari mengi ya kubeba wanafunzi, maarufu Kiingereza kwa jina la School Bus katika jiji la Dar es Salaam hayana sifa kwa kuwa ni chakavu hali inayoweza kuhatarisha maisha ya wanafunzi.Usafiri wa mabasi ya shule hasa maeneo ya mijini uliibuka kwa kasi miaka ya karibuni kwa lengo la kurahisisha usafiri kwa wanafunzi.

Hata hivyo, baadhi ya mabasi haya yamekuwa yakitumiwa kama sehemu ya kujipatia kipato kwa wamiliki wa shule huku wakishindwa kuzifanyia kazi kero mbalimbali zinazowakabili wanafunzi wanaotumia aina hii ya usafiri.
Angela Kusekwa, mkazi wa Mbezi Beach Dar es Salaam, ni miongoni mwa wazazi wasioridhishwa na mwenendo wa vyombo hivi anavyosema badala ya kuwa mkombozi kwa watoto vimekuwa kero. Miongoni mwa kero za mabasi hayo anataja kuwa ni pamoja na wanafunzi kujazwa kupita kiasi na kuchelewa vituoni.

“Mimi mtoto wangu alikuwa anasoma shule moja huko Buza sigara.Watoto walikuwa wanajazana kama nini katika gari, walikuwa wanabebana. Kwa sasa nimempeleka shule ya kulala,” anasema mzazi huyo na kuongeza:
“Wewe angalia tu, watoto wadogo wa shule nyingi tu hapa, unakuta wanaamka saa 11 alfajiri kusubiri gari la shule. Akipanda wa kwanza basi atazungushwa mji mzima na shuleni atafika saa mbili. Kurudi nyumbani atakuwa wa mwisho, akija amechoka hata kusoma hawezi, huu ni ujinga.”

Anaungwa mkono na Dastun Komba mkazi wa Tabata Bima anayesema usafiri wa wanafunzi shuleni ni sehemu ya miradi ya wenye shule kujipatia fedha. Anafafanua kwa kusema:“ Mimi mtoto wangu hajaanza shule, lakini nawaona watoto katika hayo mabasi. Mengine yalikuwa daladala sasa yapo hoi, wanayageuza kuwa mabasi ya wanafunzi. Si bure nadhani watu wanafanya biashara na ndio maana wamiliki wa shule wanalazimisha wanafunzi wapande mabasi haya.’’

Joyce Adam (jina si lake) anasoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya St. Marys, anasema tatizo la mabasi ya shule hiyo ni kuwa mengi yamechoka huku wanafunzi wakijazana kupita kiasi wakati wa kwenda shule ama kurudi nyumbani.

“Wewe usipate shida, angalia mabasi ya shuleni kwetu asubuhi wakati yanaenda shuleni au jioni wakati yanatoka, tunajazana kwenye mabasi mpaka basi,” anaeleza mwanafunzi huyo.Mwanafunzi mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini anayesoma Shule ya Sekondari ya Green Acres iliyopo Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, anasema moja ya kero kubwa za mabasi ya shule ni mizunguko mikubwa ambayo anasema inawachosha wanafunzi kabla hata hawajafika shuleni.

“Wakati mwingine bora mtu ulale tu shuleni, unaweza kukaa kwenye gari saa tatu unazunguka tu hujafika shuleni. Ukifika darasani tayari unakuwa umeshachoka. Magari yenyewe haya yamezeeka, kwa hiyo kuharibika njiani siyo jambo la ajabu,” anabainisha.

Aidha, utafiti wa umebaini kuwa baadhi ya shule zimefikia hatua ya kuingiza gharama za usafiri huo katika ada kwa lengo la kushinikiza wanafunzi kutumia mabasi ya shule.
Pia ziko shule zinazokodisha mabasi yaliyochoka hususan daladala kwa lengo la kukwepa gharama za kukodisha mabasi mazima! Kwaiyo jamani wazazi wenye watoto ebu jaribuni kuchunguza jama japo kidogo je mwanao alivyoondoka asubuhi amerudi kwenye hali gani? maana mie mwenyewe nina jirani yangu pale Home Kinondoni mwanae akirudi utamuhurumia maana Vumbi mpaka kwenye Kope na Basi likisimama kumshusha lazima Basi lichukue dk 10 kwa jinsi ''MADENTI' walivyojazwa na wengine ni wadogo kabisa hawawezi kuhimili Vishindo vya usafiri wa hayo Madaladala kwa mtindo wa kujazana kivile na mpaka wengine wanatoa vichwa vyao Nje bila uangalizi wowote, hii ni 'HATARI'' jamani...


No comments:

Website counter