Tuesday, May 3, 2011

SASA NANI MKWELI KWELI HILI 'JAMBO' JAMANI...


Ridhiwani Kikwete : Mimi si bilionea wananisingizia!
MTOTO wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwani Kikwete, amesema yeye sio bilionea na kwamba wanaomtuhumu amewapa siku saba kuanzia leo, kumwombe radhi vinginevyo atachukua hatua za kisheria dhidi yao. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Ridwiwani alitaja mali anazomiliki kuwa, ni shamba lililoko mjini Bagamoyo, lenye ukubwa wa ekari 1.5, gari ndogo aina ya Toyota Camry na akaunti kwenye benki za CRDB, Stanbic na NBC. Mkutano huo umekuja baada ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, kumtuhumu Ridhiwani kuwa ni kijana bilionea, huku Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila, akipigilia msumari kuwa mtoto huyo wa rais ni tajiri anayemiliki malori, kampuni za ujenzi wa barabara, ardhi na maghorofa ya kupangisha. “Habari hizo zimejaa uongo, ambao madhumuni yake ni kunichafua mimi na mzazi wangu (Rais Kikwete), pia wanajaribu kupandikiza chuki ili tuonekane sisi ni wabaya mbele ya jamii, nataka waniombe radhi vinginevyo nitachukua hatua za kisheria,” alisema Ridhiwani na kuongeza: “Mtikila na Slaa ni watu wazima, mimi sina kinga yoyote kisheria wathibitishe ubilionea wangu ili niweze kuchukuliwa hatua za kisheria “Nina shamba wilayani Bagamoyo lenye ukubwa wa ekari moja na nusu na gari aina ya Toyota Camry, sina maghorofa, sina malori, sina chochote zaidi ya hivyo nilivyovitaja. Pia, ninamiliki akaunti kwenye benki za CRDB, NBC na Stanbic, waandishi nendeni huko mkachunguze kiasi nilichonacho mtapata jibu badala ya kuandika porojo za akina Slaa na Mtikila.” Ridhiwani aliongeza kuwa, Dk Slaa na Mtikila ni makanjanja wa kutengeneza habari za uongo na kuwataka waandishi wa habari kuwa makini wakati wa kuripoti habari zao. Ridhiwani alisema: “Jamani waandishi wa habari hawa wazee kuweni nao makini, wanaweza kumtuhumu mtu yeyote kwa kashfa za uongo, nyinyi mkiandika tu kila wanayoeleza mnaweza kupatwa na matatizo ya kisheria katika kuthibitisha mnayoyaandika, “Nchi hii inaongozwa kwa misingi ya utawala bora na unaoheshimu haki za binadamu, natoa rai kwa Dk Slaa na Mtikila wasiwe makanjanja wa kutengeneza habari za uongo kwa lengo la kujitafutia sifa za kisiasa katika jamii. Hapa jijini kila mtu anastahili yake ya maisha, unaweza kuonekana unaendesha Benzi kumbe umeliazima, lakini watu wanaokuona wanasema jamaa ana Benzi.”Alipoulizwa kuhusu kumiliki magari za kifahari aina ya Hammer, Ridhiwani alijibu: “Sio tu kulimiliki gari hilo hata lifti sijawahi kupata, yaani sijawahi kupanda gari la aina hiyo, huo ni uzushi.” Pia, alipoambiwa aeleze kiasi cha fedha kilichopo kwenye akaunti zake kwenye benki alizozitaja alisema: “Jamani waandishi mbona mnaandika wanayoyasema akina Slaa na Mtikila, nendeni pia kwenye benki hizo mkatafute habari kujua fedha ninazomiki kwenye akaunti hizo wao ndio watawaeleza ukweli. Kuhusu tuhuma kwamba amekuwa akisafiri nje ya nchi mara kwa mara, Ridhiwani alisema tangu amemalize masomo yake nje ya nchi, hajasafiri nje na kwamba, shughuli zake zipo nchini huku akitaka kuulizwa Idara ya Uhamiaji kama anadanganya. Alisema hata yeye huwa `anachacha’ ama kukosa fedha hadi wakati mwingine hulazimika kwenda kwa baba yake kuomba msaada.“Siku nyingine hata mimi wanayeniita bilionea huwa mambo yanakuwa magumu, nina kosa fedha kabisa hadi ninalazimika kumfuata mzee (Kikwete) ili aokoe jahazi, ninaishi maisha ya kawaida kabisa,” alisema Ridhiwani.

No comments:

Website counter