Monday, April 11, 2011

KUTANA NA FUNDI 'CHEREHANI' KIPOFU KABSAAAA....
ABDALLAH NYANGALIO: Fundi stadi wa nguo asiyeona kabisaImage
Nyangalio akikata kitambaa.
 • Habari zinazosomwa zaidi:

 • HAKUNA maneno yanayoweza kufaa, zaidi ya kusema Abdallah Nyangalio ni miongoni mwa watu wenye ujasiri na uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto za maisha. Ni jasiri kwa sababu ameweza kupambana na ulemavu wa macho alioupata ukubwani, na badala yake akapambana kuhakikisha anajitafutia maisha kwa njia halali, tofauti na walemavu wengine wanaobweteka na kuishia kuwa omba omba katika maeneo mengi, hasa ya mijini.

  Yeye aligeukia ufundi wa nguo, na sasa ni miongoni mwa mafundi hodari wanaokubalika ndani na nje ya nchini. Je, ilikuwaje hata akawa katika hali ya ulemavu aliyonayo sasa? Katika mazungumzo yaliyozaa makala haya, Nyangalio anasema: “Nilipohitimu shule nilifanya biashara kwa lengo la kutafuta mtaji utakaoniwezesha kutimiza ndoto za kuondokana na umasikini, lakini niliugua na kupofuka macho hivyo kujikuta katika kundi la watu wenye ulemavu.”

  Anakumbuka kwake huo ulikuwa mtihani mkubwa, lakini hakukata tamaa ya maisha, bali alikuwa mwepesi kukubali kuishi katika hali ya ulemavu wa macho, kisha kutafuta mbinu zitakazomuwezesha kujipatia kipato ili kuepuka kuishi maisha tegemezi. Uwezo wake wa kukabiliana na changamoto za maisha ndio uliomfanya Nyangalio kuwa fundi stadi wa nguo na habari zake zimeweza kusambaa sehemu mbalimbali Afrika Mashariki na Kati kama kielelezo kwamba ulemavu sio mwisho wa maisha kwa kuwa mtu mwenye ulemavu akiwezeshwa anaweza.

  Akielezea historia ya maisha yake, Nyangalio anasema alizaliwa mwaka 1959 katika kijiji cha Kilimani, Rufiji mkoa wa Pwani akiwa hana tatizo lolote la kiafya. Alipofikisha umri wa miaka saba aliandikishwa katika shule ya Msingi Kilimani ambapo alisoma hadi darasa la nne kisha akahamia shule ya msingi Miburani, iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam. Alihitimu elimu ya msingi mwaka 1977 na kujiunga na biashara ndogo ndogo kwa kuwa wazazi wake hawakuwa na uwezo wa kumuendeleza kimasomo.

  Alifanya biashara ya nguo kwa miaka kumi huku akidunduliza mtaji kwa lengo la kufungua duka la nguo na kuimarisha biashara yake. Hata hivyo, anakumbuka mwaka 1988 alipata maumivu makali ya kichwa yaliyoambatana na kukosa usingizi. “Kichwa kiliniuma sana na nilikaa mwezi mzima bila kupata usingizi…nilipata vidonge vya usingizi, lakini havikusaidia badala yake kichwa kiliendelea kuuma na nikawa na hali ya kuchanganyikiwa,” anasema.

  Hali hiyo ilisababisha aende katika hospitali mbalimbali kutafuta tiba bila mafanikio hadi alipopata ushauri kwenye klabu ya Lions iliyoambatana na barua ya kwenda katika Hospitali ya Rufaa Muhimbili. Baada ya kufanyiwa uchunguzi katika hospitali ya Muhimbili, Nyangalio aliambiwa kuwa tatizo la kukosa usingizi linatokana na hitilafu iliyojitokeza katika mishipa ya macho na tiba pekee ni upasuaji utakaomfanya kuwa kipofu kwa maisha yake yote.

  “Nilielezwa wazi madhara ya kufanyiwa upasuaji na madaktari waliniambia nina uwezo wa kukubali au kukataa tiba hiyo….kwa kuwa niliteseka sana kwa kukosa usingizi, nilikubali kufanyiwa upasuaji,” anasema. Anaendelea kusema, “baada ya kufanyiwa upasuaji kichwa kiliacha kuuma na nilipata usingizi, lakini nilipoteza kabisa uwezo wa kuona….hata hivyo nilijipa moyo kwa kuzingatia usemi wa wahenga kwamba; hujafa hujaumbika.”

  Ingawa alijipa moyo anakiri ilikuwa vigumu kukubaliana na hali hiyo kwa sababu alishindwa kutambua mchana na usiku kutokana na kiza kinene kilichotanda kwenye macho yake. Alihofia kuishi maisha tegemezi. Hata hivyo daktari aliyemfanyia upasuaji alimfariji na kumpa nafasi ya kukaa katika hospitali ya Muhimbili kwa miezi mitatu akipewa ushauri pamoja na mbinu za kuishi katika hali ya kutoona. Anasema mbinu hizo ni pamoja na elimu juu ya maisha na changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu na jinsi ya kupambana nazo.

  Pia alifundishwa kusoma maandishi maalumu kwa watu wasioona, kutumia cherehani pia jinsi ya kukata na kushona nguo mbalimbali. Baada ya kutoka hospitalini, alikutana na changamoto nyingi katika maisha kwa kuwa baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki walimuona kama mzigo hivyo baadhi ya ndugu walilumbana wakitupiana jukumu la kumtunza. “Kabla ya kuugua nilikuwa na mke na watoto watatu….lakini hali ya ulemavu ilisababisha mke wangu kunikimbia kwa madai kuwa hawezi kukaa na mtu asiyekuwa na uwezo wa kufanya kazi,” anasema.

  Anasema awali mke huyo aliondoka na watoto wote, lakini baadaye aliwarudisha hivyo wakalelewa na bibi yao, yaani mama mzazi wa Nyangalio. “Hali ya ulemavu ilisababisha hata baadhi ya marafiki kunikimbia….namshukuru Mungu mama yangu alinifariji, pia watoto wangu walipoelimishwa juu ya hali yangu walielewa, kunikubali na kunitambua kama baba yao….jambo hilo lilinipa faraja kubwa,” anasema.

  Anasema pamoja visa na mikasa iliyompata aliweka mikakati ya kushinda changamoto katika maisha ili aweze kuudhihirishia ulimwengu kuwa binadamu ameumbwa ili aweze kukabiliana na taabu mbalimbali kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu. Aliendelea kumuamini na kumtegemea Mungu kwa kila jambo alilolifanya huku akiwa na matumaini makubwa kuwa Mungu atampa njia nyingine ya kuishi bila ya kuwa tegemezi.

  Baada ya miezi saba ya ugonjwa alirudi katika shughuli za biashara ndogo ndogo kwa kuuza nguo za mitumba pamoja na kushona nguo kwa kutumia cherehani ya jirani yake. Alidunduliza mtaji mpaka alipopata uwezo wa kununua cherehani yake na kuanza kazi ya kushona nguo mbalimbali hasa sare za wanafunzi wa shule ya msingi. Anasema baada ya kukaa miaka miwili bila mke, alipata mchumba na kuoa kwa kuzingatia kanuni na maadili ya dini ya Kiislamu.

  Pia alijiimarisha kiuchumi na kurudia maisha ya kujitegemea kama kiongozi wa kaya. “Nilifarijika sana kwa kuwa mke wangu wa sasa ananipenda kwa dhati tena alikuwa amekataa wachumba watatu na kunikubali mimi nikiwa katika hali ya ulemavu,” anaeleza. Anasema baadhi ya ndugu, marafiki na jamaa wa mke wake walipatwa na mshtuko na kujaribu kumzuia asiolewe na mtu mwenye ulemavu, lakini alishikilia msimamo wake na kuwataka kujifunza kumheshimu Mungu ambaye ndiye anayewafanya wengine kuishi katika hali ya ulemavu.

  “Msimamo wa mke wangu ulinidhihirishia ni kiasi gani anamcha Mungu, kwani hiyo ndio sifa ya kipekee niliyoitegemea…pia mama yake mzazi alimpa moyo wa kuolewa na mwanaume anayempenda na aliwakemea wale waliomcheka na kumkatisha tamaa,” Nyangalio anasema. Ingawa anakabiliwa na hali ya ulemavu, Nyangalio ana mpango wa kutimiza shauku ya mkewe ambaye hata kabla ya kuolewa alitamani kuwa mama wa watoto watano.

  “Kwa jinsi mke wangu anavyonipenda nitajitahidi kutimiza ombi lake la kuwa na watoto watano...na Mungu akijalia mwaka huu anatarajia kupata mtoto wa nne,” Nyangalio anasema. Anasema atajitahidi kuitimizia familia yake mahitaji yote, ikiwa ni pamoja na kuwapatia watoto wake elimu bora na kuwafundisha kukabiliana na changamoto mbalimbali katika maisha. Kipaji cha Nyangalio alianza kufahamika mwaka 1994 wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu wa macho maarufu kama siku ya Fimbo Nyeupe Duniani.

  “Wakati wa maadhimisho hayo mgeni rasmi alisifia suti aliyokuwa amevaa aliyekuwa kiongozi wa taasisi ya wasioona. Kisha akaambiwa kuwa suti hiyo ilishonwa na fundi asiyeona hivyo nikaanza kujulikana kuanzia siku hiyo,” anasema Nyangalio anayekumbuka kuwashonea nguo Anna Abdallah, wakati huo akiwa Waziri wa Afya, Sophia Simba, Joel Bendera na wengine wengi.

  Hivi sasa Nyangalio anafanyia shughuli zake Mbagala Kibonde Maji jijini Dar es Salaam ambako amejenga makazi yake ya kudumu. Kama ilivyo kwa Watanzania wengine, mtaji wa Nyangalio unapanda na kushuka kwa sababu fedha kidogo anazopata katika biashara yake anazitumia kwa mahitaji ya kifamilia, ikiwa ni pamoja na kutatua matatizo ya kijamii. Hata hivyo, amefanikiwa kusajili kampuni inayojulikana kama Nyangalio Fashion Centre ambayo ana mpango wa kuitumia kutoa elimu ya ufundi cherehani hususani kwa watu wasioona.

  Nyangalio amewahi kutoa elimu ya ushonaji kwa watu wenye ulemavu ambayo yalifadhiliwa na Taasisi ya Taifa ya Huduma ya Maendeleo ya Wasioona (TNIB), ambapo wanafunzi wanne walihitimu na kufaulu kwa kiwango cha kuridhisha. “Wapo wanafunzi waliohitimu mafunzo ya ushonaji, lakini hadi leo hawajaweza kutumia ujuzi wao kwa sababu ya ukosefu wa mitaji hususani vyerehani. Tatizo hilo limenipa msukumo wa kuanzisha kampuni ambayo itatoa fursa za ajira kwa vijana hususani wenye ulemavu,” anasema Nyangalio.

  Hivi sasa ana mashine mbili za kushonea ambazo anategemea kuzitumia kutoa mafunzo. Anaomba watu wenye uwezo kumsaidia ili kupata wafadhili wa kutimiza ndoto zake za kuanzisha shule ya ushonaji hususani kwa watu wenye ulemavu. Anafahamisha kuwa watu wenye ulemavu wanatumia cherehani za kawaida na kushona nguo kwa umakini wa hali ya juu kwa kusikiliza mlio wa cherehani huku wakipapasa nguo ili kuepuka kupindisha.

  “Kwa kufuatilia mlio wa cherehani unaweza kutambua kama umetoka nje ya mstari au la. Kwa kuwa watu wenye ulemavu wa macho hawaoni wako makini zaidi kwa kufuatilia sauti pia kutambua vitu kwa kuvipapasa...unajua Mungu hawezi kukunyima vyote,” Nyangalio anasema. Hutumia umakini wa hali ya juu kupima nguo kwa kupapasa kitambaa kisha kukipima kwa kutumia vipimo vinavyoweza kusomwa na watu wasioona.

  Kitu pekee ambacho mtu asiyeona hawezi kufanya ni kuchagua rangi ya vitambaa...hapo lazima asaidiwe, lakini ana uwezo wa kutambua aina ya vitambaa kama ni vya jinja, hariri, tetroni au polista bila kuambiwa na mtu. Ingawa haoni, Nyangalio ana uwezo wa kushona suti za kiume na nguzo za kike kwa mitindo mbalimbali kiasi cha kuwazidi hata baadhi ya mafundi wasiokuwa na ulemavu wa macho. Wakati wa kukata nguo hutumia sindano kuweka alama maalumu sehemu anazotaka kuweka mikunjo au vifungo.

  Pia hutumia mafundo madogo kama alama lakini mafundo hayo anakuwa madogo kiasi kwamba mtu anayeona hawezi kuyatambua kwa urahisi. Ustadi wa Nyangalio umemuwezesha kushiriki katika maonyesho mbalimbali ya ujasiriamali yaliyofanyika nchini pia katika nchi za Zambia na Kenya.

  Nyangalio anaiomba jamii kutokuwachukulia watu wenye ulemavu kama mzigo kwa kuwa gharama za kutowaendeleza na kuwafungia ndani ni kubwa ikilinganishwa na gharama za kuwaendeleza na kuwapa fursa ya kushiriki katika shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Pia anaiomba serikali kutoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu kwa kuwapatia mafunzo maalumu, vitendea kazi na mitaji ili kujenga jamii inayothamini utu na changamoto zinazowakabili watu wenye mahitaji maalumu.

  Nyangalio ni shabiki wa michezo kama soka, anafuatilia habari za kimataifa, kushiriki katika masuala ya maendeleo ya jamii na kujiendeleza kielimu. Huyo ndiye Abdallah Nyangalio ambaye hakukata tamaa baada ya kupata ulemavu, bali aligeuka kuwa jasiri kiasi cha sasa kuwa mmoja wa watu wa kupigiwa mfano. Hakuna shaka kwamba, kama atapewa nguvu ya ziada kiushauri na hata kiuchumi, anaweza kufika mbali zaidi. Nyangalio anapatikana na kwa simu namba 0783 399 846 au 0717 315 011.

  No comments:

  Website counter