Moshi Hemba Mfaume
WASWAHILI husema, ‘kazi ni kazi, bora mkono uende kinywani’, hivi ndivyo ilivyo kwa Moshi Hemba Mfaume ambaye kwa miaka 32 amekuwa akichinja ng’ombe katika machinjio ya Vingunguti jijini Dar es Salaam.
Ni kazi ambayo kwa jumla inawezekana imemwezesha kuwachinja ng’ombe 1,152,000 kwa muda wote wa kazi yake ile.
“Naipenda sana kazi yangu kwa kuwa ndio ambayo imenifanya nifike hapa nilipo kwa kuniwezesha kupata maendeleo yangu na familia yangu, japo sikuwahi kuwaza kama ningekuwa mchinjaji katika maisha yangu, lakini namshukuru mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuipata.”
Hiyo ni kauli yake mzee huyu mwenye umri wa miaka 61, mkazi wa Buguruni jijini Dar es Salaam ambaye anakiri kuwa yeye ni mchinjaji mkongwe wa ng’ombe katika machinjio hayo ya serikali.
Hemba ambaye anasema kuwa ni mzaliwa wa Kisarawe, Pwani alipata elimu ya msingi katika Shule ya Kisarawe miaka ya ‘50 ambapo alishindwa kuendelea na masomo ya darasa la tano baada ya matokeo ya darasa la nne kutokuwa mazuri.
Anasema kuwa alianza kufanya biashara ya kuuza karanga, muhogo na bidhaa mbalimbali sokoni lengo lake likiwa ni kujikimu kwa kipato, jambo ambalo lilimsaidia kufanikiwa kuendesha maisha yake ya kila siku.
Kutokana na uwezo wake mkubwa katika kucheza soka, Hemba anasema kuwa mwaka 1972 alipata ajira katika karakana ya iliyokuwa Idara ya Ujenzi, Mawasiliano na Barabara (sasa Wizara ya Ujenzi) ambako alikuwa akifanya kazi ya ufundi wa kutengeneza magari ambayo aliifanya kwa takribani miaka minne.
Anasema kuwa akiwa katika karakana hiyo alikuwa akilipwa mshahara wa Sh240 kwa mwezi, kiasi ambacho anakiri kuwa kwa wakati huo kilitosha kwa mahitaji yake ya kila siku.
“Nilipata faraja sana baada ya kupata kazi katika karakana hiyo na niliongeza bidii katika soka kwa kuwa hicho ndicho kilikuwa kigezo cha kupata ajira mahala hapo.
“Kwa bahati mbaya, mwaka 1976 timu yetu ya Ujenzi ilivunjwa na hivyo kunikosesha kazi nikaondoka na kwenda kiwanda cha nguo cha Kilitex cha mjini Arusha ambako hata hivyo sikukaa kwa muda mrefu na hatimaye nikarejea Dar es Salaam,” anasimulia.
Anasema kuwa aliporejea Dar es Salaam alijiunga na kiwanda cha Saruji cha Wazo Hill kilichoko Tegeta ambapo alikuwa akifanya kazi ya kukusanya saruji iliyomwagika, kazi za usafi na nyinginezo ambapo hata hivyo hakudumu nazo sana kwani aliamua kuachana na kazi hiyo na kutafuta kazi nyingine.
Anasema mwaka 1977 alilazimika kufanya kazi kwa kujitolea katika machinjio ya Vingunguti baada ya kuona maisha yanazidi kuwa magumu na alijitolea kwa kazi hiyo akipiga deki na kufanya usafi mwingine.
“Nilijitolea kwa miaka miwili katika machinjio haya wakati huo yakiwa chini ya Mwarabu aitwaye Salehe Dahari kabla ya serikali kuchukua vitega uchumi vyake mwaka 1979, kazi ilikuwa ngumu sana kama unavyojua kazi za watu wasio na elimu kubwa zina mateso yake,” anasema na kuongeza:
“Sikukata tamaa na nilijitolea kwa miaka miwili huku nikipata posho kidogo tu ambayo ndo ilinisukuma katika masiha yangu, lakini niliamini siku moja nitafanikiwa na maisha yangu yatakuwa mazuri kwa kuwa niliweka nia na kuipenda kazi yangu”
Hemba anasema kuwa mnamo mwaka 1979 baada ya serikali kuchukua vitegauchumi vyake ikiwamo machinjio hayo ya Vingunguti, yeye alifanikiwa kuwekwa katika ajira hasa kutokana na viongozi wake kubaini uwezo na uadilifu wake kazini.
Anasema kuwa aliwaheshimu sana wakuu wake wa kazi jambo ambalo hadi leo analifanya kwa kuwa alijua ni watu muhimu katika kufikia malengo yake katika maisha na kwamba ndio ambao walikuwa wakimshauri kwa mambo mbalimbali.
“Nilifurahi sana nilipopata kazi ya kuajiriwa kwa kuwa hicho ndicho kitu nilichokuwa nikikililia kwa siku nyingi, niliahidi kuendelea kuwa mwadilifu kazini kwa kuwaheshimu na kuwatii wakuu wangu wa kazi na kufuata sheria za kazi, hiyo ndio siri ya mafanikio yangu,” anasema
Anasema kuwa kazi ya kuchinja aliianza rasmi mwaka 1979 ambapo kwa kupewa mwongozo mzuri na Iddi Kondo Sewando alipata ujasiri wa kufanya kazi hiyo ya kuchinja ng’ombe kiasi ambacho aliwakuna watu wengi machinjioni hapo.
Anasema kuwa siku ya kwanza alipata tabu kidogo kwa kuwa alikuwa akikiona kitendo hicho cha kuchinja katika mawazo yake siku nzima na kumfanya ashtuke mara kwa mara kutokana na hisia hizo ambazo baada ya kuzoea kazi ziliondoka zenyewe kichwani mwake.
“Kama unavyojua ng’ombe ni kiumbe hai kwa hiyo unapomchinja hushtuka, siku ya kwanza hata mimi mwili ulisisimka, nilishtuka tena niliogopa, lakini kwa kuwa nilitaka kuwa na utendaji bora katika kazi yangu niliongeza ujasiri na hatimaye kuizoea kazi hiyo,” anasema
Anaongeza kuwa baaadye alibobea katika kazi hiyo na kwamba sasa anachinja ng’ombe kati ya 100 hadi 150 kwa usiku mmoja jambo ambalo kwake limekuwa ni la kawaida.
“Kila siku nachinja ng’ombe kati ya 100 hadi 150 na nimeizoea kazi hii sasa najua mbinu nyingi tu za kumchinja ng’ombe tena bila usumbufu na hivyo sio kitu cha kutisha tena kwangu,” anasema
Anasema kuwa alijawa na furaha ya ajabu baada ya kupata mshahara wake wa kwanza akiwa machinjioni hapo ambao ulikuwa ni Sh 380, pesa ambayo alikuwa hajawahi kuipata kama mshahara na hivyo pesa ilimwongezea bidii katika kazi yake hiyo.
Anasema anaipenda sana kazi yake ya uchinjaji kwa kuwa imemletea tija tofauti na kazi alizokuwa akizifanya kipindi cha nyuma na kwamba hali hiyo imemwezesha kujijenga kimaisha na kununua mahitaji muhimu ya familia.
Anasema kuwa kazi hiyo imemwezesha kujenga nyumba ya kuishi iliyoko Buguruni na kuwasomesha watoto wake wanne hadi kufikia kiwango cha elimu ya sekondari na vyuo, ambapo watoto wake wawili ni madereva wa magari wakati, mmoja mwalimu na mwingine ni nesi.
Anasema kuwa uadilifu wake kazini umemjengea heshima kubwa miongoni mwa wafanyakazi wenzake na wakuu wake wa kazi ikiwa ni pamoja na ndugu, jamaa na marafiki ambao wamekuwa wakimpongeza kwa kazi yake hiyo.
“Naishukuru familia na ndugu zangu kwa kuniunga mkono kwa kazi yangu hakuna aliyeonyesha kutoikubali pamoja na kwamba watu wengi wanaiona ni kazi ngumu na inayotia kinyaa lakini ndugu zangu wananipa faraja kwa kuwa wako nyuma yangu wakinipa nguvu ya kusonga mbele katika maisha” anasema
Anasema kuwa changamoto ambazo zinamkabili katika kazi yake ni pamoja na kupata shida ya macho kuona kutokana na madhara yanayotokana na kuona maji ya mimba ya za ng’ombe ambayo yanaathari kubwa katika macho.
Anasema pamoja na kutumia miwani maalumu ya macho lakini bado tatizo hilo ni kikwazo kwake kwa kuwa limemuathiri kwa kiasi kikubwa japo bado yupo imara katika kufanya kazi yake hiyo ya uchinjaji.
Aidha, anasema kuwa changamoto nyingine ni suala la kutopata usingizi wa kutosha hasa kwa kuwa kazi yao huwataka kuifanya kuanzia saa tano usiku hadi saa kumi za alfajiri na wakati mwingine kujikuta wakiendelea kufanya kazi za nyumbani wakati wa mchana.
Anasema zamani wakati akiishi katika nyumba za kupanga majirani zake walibaki na maswali na wengine kumhisi vibaya kuwa labda ni mwizi hasa kutokana na kufanya kazi usiku na mchana kulala huku familia yake ikikaangiza nyama kila siku.
“Changamoto nyingi ni za kawaida tu, lakini hili la madhara ya maji ya mamba za ng’ombe ndilo kubwa zaidi na inahitaji umakini zaidi vinginevyo unaweza kuishia kuwa kipofu hapo baadaye,” anasema
Hata hivyo, Hemba anawashauri vijana kujishughulisha na kuacha kusubiri kupata kazi kirahisi kama ambayo vijana wengi wamekuwa wakidhania na kukaa vijiweni kusubiri kupata kazi rahisirahisi na zenye mshahara mkubwa.
Anasema kuwa wakati anaanza yeye kazi alijitolea kwa miaka miwili na baadae kuajiriwa jamno ambalo hata vijana wa leo wanapaswa kuliiga kwa kuwa subira huvuta heri na huonyesha ukomavu na nia ya kazi husika.
“Vijana wanapaswa kutambua kuwa huu sio wakati wa kuzembea kusubiri kazi rahisi rahisi tena zenye mshahara mkubwa, mimi nilianza kuuza karanga, kufanya kazi kwenya mashirika kama kibarua na hatimaye sasa niko hapa machinjioni ni matunda ya uvumilivu wangu” anasema Hemba
Aidha Hemba anawashauri vijana ambao watapenda kufanya kazi ya uchinjaji wanaweza kufika katika machinjio hayo kwa kuwa kuna mafunzo mbalimbali huwa yanatolewa kwa vijana kwa ajili ya kuandaa wachinjaji wa kizazi kijacho.
“Baada ya kuifanya kazi hii kwa miaka 32 ninatarajia kustaafu kazi hii mwakani, kwa hiyo ni vizuri kupata vijana ambao wataendeleza fani hii na kuna mafunzo mengi yamekuwa yakiendeshwa na asasi mbalimbali za kiraia juu ya namna ya kuchinja kwa ubora zaidi kwa hiyo vijana wasisite kujitokeza ili kujifunza,” anamalizia.
No comments:
Post a Comment