Saturday, April 16, 2011

HII NI HADITHI YA KWELI KWA WALE WOOOTE WANAOTAKA KWENDA LOLIONDO KWA 'BABU'...


Hii ni hadithi ya ndugu yangu mmoja aliyekwenda LOLIONDO majuzi. Anasimulia hivi, ni usiku wenye baridi kali, mvua inayoambatana na upepo inanyesha. Katika hali ya kawaida, baridi hii haivumiliki kwani nawaona kina baba wakiota moto katika jiko linalotumiwa na mama lishe.Natamani kuungana nao lakini nashindwa kwani jiko lenyewe ni dogo na idadi ya watu waliolizunguka ni kubwa. Lakini pia ugeni wangu katika eneo hilo unakuwa kikwazo cha shauku yangu ya kujiunga nao.Mbele yangu nawaona kina mama na watoto wao wengi kiasi, wakiwa wamelala barazani katika moja ya nyumba za wageni zilizopo katika eneo liitwalo Wasso.Wasso ni kitongoji maarufu katika eneo la Loliondo. Kitongoji hiki ni sehemu ya mji wa Loliondo na kwa mujibu wa wenyeji wa mji huu, Wasso ni mji mpya unaopanua ukubwa wa mji wa asili wa Loliondo.Eneo hili linachangamshwa na uwepo wa shughuli nyingi za kibiashara, nyumba za wageni na hata gulio kubwa ambalo hufanyika kila Jumamosi likiwavuta wafanyabiashara wengi kutoka nchini Kenya. Lakini usiku, halitamaniki kutokana na baridi kali.Katika baraza au kwenye veranda ya nyumba ya kulala wageni iitwayo Sayi, ndipo walipolala kina mama hawa. Udadisi wangu unabaini kuwa hawa ni wenyeji wa maeneo ya Wilaya ya Ngorongoro na wako safarini kwenda Samunge kwa Mchungaji Ambilikile Mwasapila kunywa dawa.“Usiku umewakuta hapa hivyo lazima walale halafu kesho asubuhi na mapema, wanaamka kwenda kwa babu kunywa dawa," anasema mmoja wa wahudumu wa nyumba ya wageni aliyejitambulisha kwa jina moja la Fatma na kuongeza: “Hapa ni kawaida, tena leo wamepungua, huwa wanakuwa wengi hadi tunawatimua (kuwafukuza). ”Nilimwuliza Fatma kwamba watu hawa wanatumia usafiri gani kwenda Samunge? Jibu lake lilikuwa ni fupi tu kwamba “…..hawa wanatembea”. Umbali kutoka Wasso hadi Samunge ni karibu kilometa 70 lakini, kwa mujibu wa wenyeji, matumizi ya njia za mkato huwawezesha kupunguza umbali huo hadi kufikia kilometa zisizopungua 40.Kwa maana hiyo wenyeji wanasema hutumia muda wa kati ya saa tano hadi sita kufika Samunge na baada ya kupata kikombe cha babu huanza tena safari ya kutembea kurudi makwao. Ng’ambo ya barabara kutoka ilipo nyumba hii ya wageni ya Sayi, ipo nyumba nyingine ya kulala wageni iitwayo Selemani. Hivyo jibu la Fatma lilinipa wajibu wa kuvuka barabara ili kwenda kuona iwapo kuna watu wengine waliolala barazani.Hali niliyoikuta ni ileile. Kina mama kwa kina baba walikuwa wakihangaika kujisitiri kwa mashuka na makoti waliyokuwa nayo. Katika hali ya ubinadamu, nawahurumia lakini sina la kufanya kwani hata kama ningekuwa na fedha za kugharamia malazi yao, vyumba katika nyumba za wageni zilizopo Wasso zilikuwa zimejaa. Malazi kwa Babu Samunge Wakati fulani nikiwa Loliondo, nililazimika kulala katika Kijiji cha Samunge ambako Mchungaji Mwasapila anatoa dawa ya magonjwa sugu.Siku ya kwanza tulipoamua kwamba tutalala Samunge mimi na wenzangu, Mussa Juma na Fidelis Felix tuliazimia kutafuta sehemu ya kulala usiku ule. Wakati tukiwa katika harakati za kutafuta malazi, nilibaini kwamba watu wengi ambao wanasubiri zamu za kunywa dawa hawana mahali pa kulala. Wengi wamechukua mikeka mabusati na kuyatandika pembezoni mwa magari yao na kulala hapo. Wengine wamekuwa katika foleni, wakilala kwa ‘staili’ hii kwa muda wa siku sita au zaidi.Lakini hawa wana ahueni kwani wana uwezo wa kufanya hivyo. Kuna wengine ambao maisha yao ni magumu zaidi ya haya. Hawa wanalala kwenye magari hasa magari makubwa kama malori mengine yakiwa ni Fuso. Humo kuna watu ambao wako taabani. Hawa hawalioni jua kwani hawana uwezo wa kutoka nje. Kutwa, kucha wamo ndani ya magari yao wakisogea taratibu kuelekea kwa Mchungaji Mwasapila.Katika gari mojawapo aina ya Fuso lililokuwa likitokea mkoani Mara, kulikuwa na abiria wasiopungua 100, wakiwemo wazee, watoto na wagonjwa ambao walikuwa hawajiwezi. Lakini pamoja na adha hiyo, watu wote katika eneo hilo wanavumilia tabu hizo wakiwa na shauku kubwa ya kukutana na Mchungaji Mwasapila ili awape kikombe. Kambi za mahemaKatika kutafuta malazi, tuliingia katika eneo lenye mahema na kuanza kuulizia gharama za kukodi kwa usiku mmoja.Katika eneo la kwanza tulionyeshwa mahema ya aina tatu. Moja ni hema ambalo kulala kwa usiku mmoja gharama yake ilikuwa Sh60,000. Hema hili ni kubwa na lina magodoro mawili madogo ya shule (futi mbili na nusu kwa tano).Pia tukapelekwa kwenye hema lenye ukubwa wa kati ambalo lilikuwa na godoro moja dogo. Gharama yake ni Sh45,000.Hema la tatu lilikuwa dogo na gharama yake ni Sh35,000. Hema hilo lilikuwa na godoro moja ndani. Kwa kuangalia uwezo wetu kifedha, tulilazimika kutafuta eneo jingine na baada ya kuzunguka katika maeneo kadhaa, tulibahatika kupata hema kwa gharama ‘nafuu’ ya Sh25,000. Hema hilo kwa mujibu wa msimamizi wake, lilikuwa na uwezo wa kulaza watu watatu kwa wakati mmoja. Katika eneo lile kulikuwa na mahema yasiyopungua 20 na wakati tulipofika, saa 4.20 usiku, lilikuwa limebaki hema moja tu, ambalo ndilo tulilopewa na kulipa kiasi hicho cha fedha. Hema hili liligeuka kuwa makazi yetu ya muda kwani kila tulipofika kulala Samunge katika siku zote 14 tulizokaa Loliondo, tukiendelea na kazi zetu za kihabari, tulikuwa tukilitumia. Usiku wa taabuUsiku wa kwanza ulikuwa wa tabu kwetu kutokana na hema hilo kuwa na dogoro moja tu dogo. Ilibidi tuweke vichwa na sehemu ya viwiliwili vyetu kwenye godoro hili huku sehemu ya miili yetu ikibaki chini katika ‘sakafu’ ya hema hilo ambalo kwa jinsi lilivyotengenzwa ni kama suti kuanzia sakafu, kuta mpaka paa. Hatukuwa na shuka, blanketi, kanga wala kitenge kwa ajili yakujisitiri na baridi. Pamoja na kwamba Samunge si sehemu yenye baridi ya kutisha, lakini ulipofika usiku wa manane, tulilazimika kuyatafuta majaketi na makoti yetu.Baridi ilianza kuingia katika miili yetu kwa mbali. Kweli, ulikuwa ni usiku wa tabu na kila mmoja wetu alitamani kuche haraka ili tuweze kuondokana na adha hiyo. Haya yalithibitika asubuhi pale kila mmoja wetu alipokuwa akiusimulia ‘usiku wake’ ulivyokuwa. Ulifika wakati tukataka kuweka azimio la kutolala tena Samunge lakini, kwa jinsi mazingira yalivyokuwa, azimio hili halikutekelezeka kwani tulirejea kulala kijijini hapa mara tatu zaidi.Hali hii inanikumbusha usiku wa mvua na baridi kule Wasso ambako kina mama na watoto wao walikuwa wamelala barazani baada ya kukosa malazi. Nilijiuliza moyoni, ikiwa sisi ambao tumepata hema tunapata tabu kiasi hicho, hali ilikuwaje kwa wale waliolala nje bila hata ya kuwa na nguo ya kujisitiri?Pamoja na hali hii, watu bado walionekana kuwa na shauku kubwa ya kufika Samunge kupata kikombe kwa Mchungaji Mwasapila.Mwisho

No comments:

Website counter