Thursday, February 3, 2011

WANAWAKE NAO WANAWEZA BWANAA ALAAAH...

RITA CHIBOMBO MDUMA: Dereva treni aliyebobea Send to a friend


RITA CHIBOMBO MDUMA


ULE mtazamo wa jamii unaotofautisha kazi za kike na za kiume hivi sasa umeanza kutelekezwa baada ya wanawake wengi kujitosa na kufanya vizuri kazi ambazo zilidhaniwa kuwa ni za wanaume pekee.

Rita Mduma(29), anathibitisha mabadiliko haya kwa kujitosa katika kazi ya dereva wa treni. Mwanamke huyo ameajiriwa na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) kama dereva ambaye anaendesha treni ya abiria kutoka Dar es Salaam hadi Zambia.

Rita anasema awali alikuwa na ndoto za kuwa mwanahabari lakini ikafutika, badala yake alitamani kuwa mwanajeshi. “Hata hivyo, sikutimiza matarajio yangu, badala yake nikasomea Usimamizi wa Hoteli na kuajiriwa katika fani hiyo, lakini ghafla nikabadili mwelekeo kwenda kujifunza udereva wa treni,” anasema Rita.

SWALI: Unasema ulitamani kuwa mwanahabari kisha kuwa mwanajeshi baadaye ukawa msimamizi wa hoteli na sasa hivi ni wewe ni dereva wa treni, ilikuwaje?
JIBU: Katika maisha yangu sikuwahi kufikiria kuwanitafanya kazi hii, ingawa nilikuwa mtundu kupita kiasi. Hata hivyo, kwa kuwa mimi ni mwenyeji wa Morogoro nilikuwa nikitumia usafiri wa treni mara kwa mara na nilivutiwa na dereva wa kike wa wakati ule aliyeitwa, Teresia Mahagatila.

Baada ya kumaliza kidato cha sita, nilisomea kozi ya usimamizi wa hoteli, katika chuo cha ‘The Global College’ na kuajiriwa hapo hapo. Siku moja niliona tangazo la nafasi mbalimbali za kazi hapa Tazara, nikaamua kupeleka maombi yangu, nikaitwa kwenye usaili na kwa uwezo wa Mungu nikafanikiwa.

SWALI: Umesema Tazara walitangaza nafasi za kazi gazetini, wewe ulivutiwa na nafasi gani?
JIBU: Kwa kuwa tayari nilikuwa nimeshahamasika na Teresia, nikaona nipeleke maombi ya nafasi ya udereva, nilijisikia kuipenda kazi hiyo kwa moyo wangu wote.

SWALI: Wakati wa usahili walikuwa na wanawake wengine walioomba nafasi kama yako?
JIBU: Tulikuwa wanawake wawili tu kati ya watu 30 tulioitwa kwenye usahili, baada ya hapo nilifaulu na hata mwenzangu anayeitwa Joyce John alifaulu vizuri. Tukapelekwa kwenye mafunzo ya udereva wa treni kwa miaka miwili katika Chuo cha Tazara kilichoko Mpika, Zambia.

Baada ya kumaliza mafunzo ya nadharia tulienda kwenye mafunzo ya vitendo Mbeya, Tanzania kabla ya kupangiwa vituo vya kazi. Mimi nilipangiwa safari za Dar es Salaam mpaka Kisaki Morogoro na hatimaye nikawa dereva kamili anayejiamini.

SWALI: Ni changamoto gani unakutana nazo uwapo kazini?
JIBU: Wakati mwingine treni likaharibika usiku njiani tena katikati ya mbuga, inakubidi ulale na abiria hadi asubuhi msimamizi wa treni atakapokuja na kurekebisha tatizo. Wakati mwingine tunalala njiani kwa wiki nzima bila kurudi nyumbani.

Swali: Baadhi ya watu wamekuwa wakichagua kazi na kuangalia kipato zaidi, unasema nini juu ya hili?
Jibu:Kazi hii ni ngumu lakini naipenda sana na imeniletea mafaniko makubwa, kwani sasa hivi najimudu kimaisha, napangilia mambo yangu na ninajitegemea. Siangalii ugumu wake bali mkono kwenda kinywani na jinsi ninavyoipenda.

SWALI: Mnapata changamoto gani mnaposhirikiana na wanaume katika kazi hii?
JIBU: Nikiwa nao sioni tofauti yoyote, tunafanya kazi kwa ushirikiano, utani mwingi sana hivyo sioni tatizo lolote kufanya kazi na wanaume.

SWALI: Nini matarajio yako kwa siku za usoni?
JIBU: Kuwa dereva wa kimataifa, tofauti na sasa naitumikia Tanzania pekee.

SWALI: Unawashauri nini wanawake wa kitanzania?
JIBU: Wanawake wanaweza kufanya kila kitu wasipobweteka. Mimi ninaamini kuwa hakuna kazi ya mwanaume au ya mwanamke, kinachotakiwa ni maamuzi na kuachana na kasumba.

Rita alizaliwa Sharifu Shamba, Ilala, jijini Dar es Salaam , lakini asili yake ni kutoka Mahenge, mkoani Morogoro. Ni kitinda mimba kati ya watoto wanane wa familia ya marehemu mzee Justus Chibombo na Alnardo Itatiro.

Amesoma shule ya msingi Msimbazi, Sekondari ya Mwanga mkoani Kilimanjaro na sekondari ya Jiteemee, baadaye alisomea usimamizi wa hoteli katika chuo cha Global jijini na mafunzo ya udereva za treni katika Chuo cha Tazara Mpika, Zambia. Mama huyo ameolewa na Andrew Mduma.

2 comments:

Anonymous said...

keep it up sister..

Anonymous said...

keep it up sister..

Website counter