Saturday, February 12, 2011

EBWANAE EBU TUAMBIE NI LINI ITAKUWA MWISHO WA MGAO WA UMEME JAMA ALAAH...


Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja



WABUNGE wa upinzani jana walimbana Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja wakitaka atoe tamko la Serikali kuhusu tatizo la mgawo wa umeme unaoendelea, hali iliyomlazimu Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuingilia kati na kumuokoa.

Hali hiyo ilijitokeza jana wakati wa kipindi cha maswali na majibu ambapo ilikuwa zamu ya Wizara ya Nishati na Madini kuulizwa huku mmoja wa wabunge waliombana Ngeleja akiwa Kiongozi wa Upinzani bungeni na Mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe.

Mbowe alisimama na kutaka kauli ya waziri ambapo kiongozi huyo wa upinzani aliuliza swali la nyongeza baada ya Ngeleja kutoa majibu juu ya matatizo ya malipo ya wafanyakazi wa mgodi wa Kiwira, ambao wanalalamikia malipo yao.

"Suala la umeme ni janga la kitaifa ambalo halitakiwi kuchukuliwa kwa mzaha, namwomba Waziri aliambie Bunge lako tukufu pamoja na Watanzania wote, ni lini hasa mgawo wa umeme utakwisha na atoe tamko la Serikali kuhusu tatizo hilo," alisema Mbowe.

Hata hivyo, wakati Ngeleja akisimama kutaka kujieleza baada ya swali hilo la Mbowe, Spika wa Bunge Anne Makinda alisimama na kumtetea Ngeleja akitaka asitoe majibu.

Alimtaka waziri huyo kutafuta muda muafaka wa kujibu swali hilo akisema kuwa halitakiwi kujibiwa kwa haraka kutokana na kugusa zaidi masilahi ya Taifa.

"Mheshimiwa Waziri, suala kama hili halitakiwa kujibiwa kwa haraka naomba uandae kauli ya Serikali juu ya jambo hili na utakuja kuliambia Bunge na wananchi na iwe kauli ya mawaziri. Hivyo usilijibu kwa haraka kwa leo," alisema Makinda.

Kauli hiyo ya Makinda, ilionekana kuwa ukombozi kwa Ngeleja kutoka kwa wabunge wa upinzani walioonekana kuikamia hoja hiyo.

Awali, Naibu Kiongozi wa Upinzani na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, alisema hali ya umeme nchini ni mbaya akitolea mfano wa juzi ambapo nchi nzima ilikosa umeme kwa saa mbili huku Tanesco ikiwa na upungufu bwa zaidi ya megawati 270.

Alisema: "Ni vigumu kusubiri, mchakato, mchakato kila siku majibu ambayo hayaridhishi, umefika wakati Serikali ichukue hali hii (kukosa umeme) kama janga la taifa".

Hata hivyo Ngeleja akijibu hoja hiyo ya Zitto ambayo ilikuwa katika swali lake la msingi, alikiri kuwa umeme ni janga la taifa.

Alisema kuwa mbali ya kuwa janga la Taifa, Watanzania wana hasira kila wanaposikia tukitaja masuala ya umeme huku akisema serikali inalifanyia kazi ili kuondokana na upungufu huo uliokithiri.

Katika swali la msingi, Zitto alitaka kujua ni kwa nini Serikali haijawalipa wafanyakazi wa mgodi wa Kiwira madai yao ambayo yamekuwa ni ya muda mrefu pamoja na kuhoji Serikali ina mpango gani kuharakisha mchakato wa mgodi huo kuchukuliwa na shirika la NSSF.

Zitto pia alitaka serikali itoe tamko juu ya upungufu mkubwa wa umeme kwa Megawati 270 ambao umeanza juzi huku kila kauli ya waziri huyo ikieleza kuwa mambo yapo katika mchakato.

Zitto alihoji ni lini masuala ya michakato yatakwisha ili Watanzania waendelee kunufaika kwa rasilimali zao.

Ngeleja alisema dhamira ya Serikali kufanikisha mgodi wa Kiwira yapo pale pale na kueleza kuwa katika kupunguza makali ya mgao huo, tayari wizara yake imenunua mafuta kwa ajili ya kuendeshea mitambo ya IPTL.

Hata hivyo, Ngeleja alisema suala hilo halikwepeki na akilinganisha na mataifa yaliyoendelea akisema mara nyingi hukukumbwa na matatizo kama ambayo yameikukumba Tanzania.

Muda mfupi baada ya kipindi cha maswali na majibu kuisha, Mwenyekiti wa kamati ya Nishati na Madini, Januari Makamba aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kuelezea kuwa hali ya umeme nchini ni mbaya.

Makamba alisema kutokana na hali hiyo alimuomba Spika wa Bunge kuiruhusu kamati yake kuanza kazi kabla ya muda wake na kuendelea na vikao mara baada ya bunge kumaliza mkutano wake Februari 18, Jijini Dar es Salaam.

Alisema tayari Spika ameiruhusu kuanza kazi pamoja na kufanya ziara katika vyanzo vya umeme ambapo kesho kamati hiyo itakwenda kutembelea Bwawa la Mtera kujionea hali halisi.

Makamba alisema kamati yake itafanya kazi kwa uwazi na kwamba serikali lazima iweke uwazi na ukweli katika mijadala na uamuzi kuhusu nishati.

"Ingawa hatuwezi kusema kamati yetu inamaliza mgao wa umeme wiki mbili zijazo, lakini sisi tutafanya kazi kwa uwazi na ukweli, Serikali nayo iweke uwazi na ukweli katika hili si kueleza michakato na miradi isiyotekelezeka kila siku," alisema Makamba.

Alisema inawezekana tatizo ni woga wa kufanya uamuzi katika masuala ya nishati na kwamba kamati yake haitasita wala kuogopa kufanya maamuzi yatakayokuwa na manufaa kwa taifa kuhusu Nishati na Madini.

Kwa mujibu wa Makamba, kamati zilizopita zilijitahidi kufanya kazi ingawa hazikuzaa matunda yanayoonekana na kwamba yeye na kamati yake wataanzia palipo na mazuri ya kamati iliyopita.

No comments:

Website counter