Mtandao wa WikiLeaks wamlipua Mattaka | Send to a friend |
|
Mtandao wa habari za kiuchunguzi wa WikiLeaks, umeendelea kuanika siri za ufisadi nchini na mara hii umemlipua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), David Mattaka.Taarifa hizo kupitia WikiLeaks zimekuja karibu wiki mbili tangu kutolewa hadharani kwa taarifa nyingine zinazohusu Mkururugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah, akidaiwa kufichua siri za Rais Jakaya Kikwete kwamba kiongozi huyo wa nchi asingependa vigogo serikalini kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa. Lakini juzi taarifa zilizoripotiwa na mtandao huo na kunukuliwa na gazeti la New York Times zimedai kuwa Mattaka anatumia mpango wa serikali wa kulifufua upya shirika hilo kwa kununua ndege mpya, kujinufaisha. Habari zimeeleza kuwa katika kufanikisha hilo, Mattaka anadaiwa kutaka kumtumia mfanyabiashara wa Kiasia ambaye anajihusisha na biashara za hoteli kuwa wakala wa ununuzi wa ndege hizo baina ya ATCL na Kampuni ya Boeing ya nchini Marekani. Tuhuma hizo dhidi ya Mattaka ziko kwenye taarifa za siri za mawasiliano za ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam, zilizoripotiwa na mwanadiplomasia wa Marekani, Dk Purnell Delly. Delly pia ndiye aliyetajwa katika taarifa za awali na mtandao wa WikiLeaks kwamba alifanya mazungumzo na Dk Hosseah. Jana Mattaka alikiri shirika hilo kukubali kununua ndege za kampuni ya AirBus ya nchini Ufaransa, lakini akapuuza madai ya kutumia wakala kwa nia ya kujinufaisha. "Huu ni upuuzi. Sikumbuki kufanya jambo hilo na tuhuma hizo hazina mashiko," alisema Mattaka alipokuwa akizungumza na gazeti dada la Mwananchi, The Citizen. Taarifa hiyo inamnukuu Delly akituma taarifa nchini kwake inayoilalamikia Tanzania kwamba ilikuwa na mbinu chafu ziliokuwa zikipangwa kuhakikisha kwamba ATCL inanunua ndege kutoka Kampuni ya Airbus ya Ulaya badala ya Boeing ya Marekani, hasa baada ya uongozi wa Boeing kukataa kutumika kwa mawakala. Kwa mujibu wa taarifa hizo, Kampuni ya Boeing iliwasilisha mapendekezo yake kwa ATCL sambamba na yale yaliyowasilishwa na kampuni ya Airbus, lakini wanalalamika kwamba kulikuwa na mpango wa makusudi wa upendeleo ambao unaashiria kwamba kulikuwa na “harufu ya rushwa”. Taarifa hiyo imedai kuwa ushauri wa Mattaka kumtaka Rob Faye, ambaye ni Mkurugenzi wa Mauzo wa Kanda ya Afrika wa Boeing kuwasiliana na mfanyabiashara na tajiri wa Kiasia ili aweze kumsaidia kufungua milango ya biashara hiyo kwa serikali ya Tanzania “haukuwa wa kawaida”. “Faye aliukataa ushauri huo kwa malezo kwamba kampuni ya Boeing haitumii mawakala katika biashara zake, siyo tu Tanzania, bali katika nchi yoyote duniani,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza: “Mawakala na malipo ya kamisheni ni kiini cha vitendo kadhaa vya rushwa ikiwemo ile ya rada ambayo Serikali ya Tanzania ililipwa asilimia 31 ya gharama kama kamisheni”. Kwa mujibu wa taarifa za mawasiliano baina ya uongiozi wa Boeing, ATCL na Ikulu, Rais Jakaya Kikwete “hakufurahishwa” na taarifa kwamba baadhi ya maafisa wa ATCL walitaka kujinufaisha wenyewe na mpango huo wa ununuzi wa ndege. Agosti 9, 2007, Faye alikutana na aliyekuwa Naibu Waziri wa Miundombinu, Dk Maua Daftari na Mkurugenzi wa Usafirishaji na Mawasiliano, Dk Bartholomew Rufunjo,ambao walimpa matumaini kwamba kusingekuwa na upendeleo katika mchakato wa ununuzi wa ndege hizo. Baadaye Agosti 10, Mattaka, alimhakikishia Faye kwamba ATCL haikutumia mawakala katika ununuzi wa ndege zake, kauli ambayo Mattaka aliirudia mara kadhaa wakati wa kikao baina ya Bodi ya Wakurugenzi wa ATCL na Faye. Faye alinukuliwa akisema kuwa huenda kumekuwa na mwasiliano baina ya Ikulu na Wizara ya Miundombinu ili kuhakikisha kwamba hakuna “mtu wa kati” katika mchakato huo. Hata hivyo, Mattaka anadaiwa kumwambia Faye kwamba kulikuwa na shinikizo kutoka ubalozi wa Marekani nchini ili Boeing wapewe nafasi ya kuuza ndege zake ATCL. Wasiwasi kwamba hakukuwa na uwazi katika mchakato huo unatokana na tangazo la aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge la Septemba 2, 2007 lililonukuliwa na vyombo vya habari kwamba Tanzania iko katika mpango wa kununua ndege mpya kutoka kampuni ya Airbus. Kauli hiyo ya Chenge ilitolewa saa 48 tangu aliyekuwa balozi wa Marekani nchini, Michael Retzer kuondoka kurejea nchini kwake baada ya muda wake wa kukaa nchini kumalizika. Hata hivyo, Chenge anadaiwa kukana kauli yake kwa kusema kwamba alinukuliwa visivyo na vyombo vya habari Septemb 7, 2007 katika kikao chake na Pully pamoja na ofisa wa uchumi katika ubalozi wa Marekani. |
No comments:
Post a Comment