|  
  RAIS  Jakaya Kikwete, amemteua Jaji Mohamed Chande Othman, kuwa Jaji Mkuu wa  Tanzania.Jaji Othman, anachukua nafasi ya Jaji Augustino Ramadhan  anayestaafu leo kwa mujibu wa sheria.
 
 Taarifa iliyotolewa jana na  Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ilisema Jaji Othman ataapishwa leo  Ikulu na ataanza rasmi kazi kesho.
 
 "Jaji Othman ataapishwa kesho  (leo) saa 4:00 asubuhi, Ikulu jijini Dar es Salaam," ilisema sehemu ya  taarifa hiyo iliyosainiwa na Mwandishi Msaidizi wa Rais, Premy Kibanga.
 
 Kabla ya uteuzi huo, Jaji Othman alikuwa ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania
 
 Jaji  huyo pia amewahi kufanya kazi katika nafasi mbalimbali za kitaifa na  kimataifa ikiwa ni pamoja na kuwa  Makamu wa Mwendesha Mashtaka wa  Mahakama ya Rwanda, iliyoko jijini Arusha.
 
 Pia amewahi kushika  nafasi sawa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali huko Timor Mashariki katika  kipindi cha kati ya mwaka 2000 na mwaka 2001.
 
 Halika kadhalika,  amewahi kufanya kazi katika Shirika la Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa  Mataifa (UNDP) na Chama cha Msalaba Mwekundu.
 
 Mwaka 2006 Jaji  Othman, alikuwa ni mmoja wa makamishna wa Baraza la Haki za Binadamu  nchini Lebanon kufuatia mgogoro kati ya Lebanoni na Israel.
 Novemba  mosi mwaka 2009, Jaji Othman aliteuliwa kuwa mtaalamu binafsi  juu ya  hali ya Haki za Binadamu Kusini mwa Sudan, jukumu ambalo atalishikilia  hadi Agosti mwakani.
 Jaji Othman alizaliwa Januari mosi mwaka  1952 na alipata Shahada ya Kwanza ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es  Salaam na Shahada ya Uzamili (MA) katika Chuo Kikuu cha Webster,  Geneva-Uswisi.
 
 Jaji Othman anakuwa Jaji mkuu wa tano mzalendo.
 
 Jaji wa kwanza mzalendo nchini alikuwa Jaji Agustine Said aliyekuwa anatambuliwa kama Baba wa Mahakama.
 
 Jaji  Saidi alifuatiwa na Jaji Francis Nyalali na Jaji Barnabas Samatta  alikuwa Jaji Mkuu wa tatu akifuatiwa na Augustino Ramadhan, ambaye  amemwachia Jaji Othman mikoba hiyo.
 
 Juzi Jaji Ramadhan alitoa  ushauri kwa mrithi wake kwamba anapaswa kujipanga ipasavyo ili matatizo  mbalimbali za Idara  ya Mahakama.
 
 Akizungumza katika sherehe za  kumuaga iliyoandaliwa na Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam  Jaji Ramadhan alisema kuna mgawanyiko mkubwa katika muhimili huo wa  serikali na kwamba hali hiyo  ni hatari katika utoaji wa hukumu za haki.
 
 Akielezea  uzoefu wake wa miaka mitatu na nusu kama Jaji Mkuu wa Tanzania, alisema  kuendelea kuwepo kwa makundi miongoni mwa majaji, kunazidisha uwezekano  wa kutotenda haki.
 
 "Kuna baadhi ya majaji katika vyombo vya  sheria ambao kati yao, kuna wanaojiona kuwa wako juu kuliko wengine na  hivyo hawapendi kushirikiana na wenzao ambao bado si wazoefu, achilia  mbali jamii ambayo wanaitumikia," alisema Jaji Ramadhan.
 
 Alisema  nafasi ya Jaji mkuu ni kubwa na ndio sura ya chombo cha sheria ambacho  majaji waliochini yake, wanapaswa kuiga mifano yake.
 
 Jaji  Ramadhan ambaye alijielezea kama mtu anayemwogopa Mungu, alisema katika  kipindi chote cha uongozi wake aliweza kujichanganya na watu wa kila  aina, jambo lililomfanya agundue kuwa kuna baadhi ya majaji nchini  hawatendi haki katika hukumu wanazotoa.
 
 Alisema kuna kipindi  alilazimika kuingilia kati hukumu za kesi mbili ambazo kwa mujibu wa  Jaji Ramadhan, hazikuamuliwa kwa haki na kwamba  hukumu hizo zilitolewa  kwa ajili ya kulinufaisha kundi la watu fulani.
 
 Jaji Ramadhan  aliweka wazi kuwa kuna madudu mengi yanayofanyika kwenye Mahakama ya  Rufaa kwani baadhi ya ushahidi unaotolewa huwa ni wa kupikwa na kwamba  ni jukumu la Jaji mkuu kuingilia kati  kila mara hali hiyo inapotokea.
 
 Jaji  Mkuu  huyo alikumbushia tukio lililotokea wakati walipokuwa katika  kikao kilichowakutanisha majaji wote wa Mahakama Kuu na Mahakama ya  Rufaa na kuelezea mtafaruku wa kurushiana maneno ulivyozuka baina ya  jaji mmoja wa Mahakama Kuu na mwingine wa Mahakama ya Rufaa.
 
 Alisema  pia kuna ushirikiano mdogo miongoni mwa majaji katika mahakama hizo  kubwa hapa nchini na kuelezea mfano wake alipokuwa akifanya kazi katika  Mahakama ya Rufaa.
 
 "Kama Jaji wa Mahakama ya Rufaa, baada ya  kuandika hukumu nilitakiwa kuigawa pia kwa wenzangu wawili waliokuwa  wakisikiliza kesi hiyo, lakini jaji mmoja alichelewa kuchukua nakala ya  hukumu hiyo, na hata alipokumbushwa alionyesha kutokujali," alisema Jaji  Ramadhani na kuongeza kuwa ilimbidi aipeleke nakala hiyo kwa Katibu wa  Jaji huyo.
 
 "Kama kunakuwa na hali hiyo ya kukosa ushirikiano  miongoni Mwa wafanyakazi wa mahakama, unadhani haki itatendeka  kirahisi," alihoji Jaji Ramadhani na kutoa wito kwa atakayeshika nafasi  yake, kulishughulikia jambo hilo.
 
 Alisema ofisi ya Jaji mkuu   lazima iwe wazi muda wote na iwe inayofikika kirahisi na wananchi kwani  kumekuwa na matukio mengi ya ukiukwaji wa haki katika chombo hicho.
 Jaji  huyo anayemaliza muda wake alisema katika kipindi cha uongozi wake, kwa  kiasi kikubwa amefanikisha kuboresha uhusiano kati ya serikali, bunge  na mahakama kwa sababu  mihimili inapaswa kufanya kazi kwa pamoja kwa  maendeleo ya nchi.
 Alifafanua kuwa ili kuhakikisha uhusiano kati  ya mihimili hiyo  unakuwepo, aliwaalika rais na spika wa bunge  kuhudhuria siku ya kimataifa ya sheria.
 | 
No comments:
Post a Comment