Baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ardhi Dar es Salaam, wakiimba nje ya jingo la Utawala katika siku yao ya kwanza ya mgomo wakishinikiza serikali kutatua kero kumi zinazowakabili, ikiwemo ya upungufu wa wahadhiri na uhaba wa mabweni. KWA muda mrefu sasa wanafunzi katika baadhi ya vyuo vikuu nchini wamekuwa katika migomo ili kuishinikiza Serikali kusikiliza matatizo yao na kuyatafutia majibu. Hivyo, wamesema kwa kuwa mamlaka husika zimetia pamba masikioni, njia pekee iliyobaki ni kugoma, kwa maana ya kutoingia madarasani. Ni kwa sababu hiyo tumeshuhudia habari za migomo katika vyuo hivyo zikitawala kurasa za vyombo vya habari katika muda wa wiki mbili zilizopita. Na katika kuchunguza kwa kina kuhusu kiini cha matatizo ya wanafunzi hao, moja ya mambo yanayojitokeza ni kuwa matatizo hayo yanafanana kwa kiasi kikubwa na karibu yote yanaelekezwa kwa Serikali. Matatizo hayo yalianzia katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), ambapo wanafunzi wa chuo hicho walivamia ofisi za bodi inayotoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu (HELSB), wakitaka bodi hiyo iwaongeze fedha ili kufidia kiwango cha ada iliyoongezwa na uongozi wa chuo hicho, lakini waliambiwa kuwasilisha malalamiko yao katika wizara husika. Wizara hiyo ilisalimu amri na kuahidi kumaliza matatizo yao. abla vumbi la sakata la IFM halijatulia, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro na Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (Kampasi ya Tanzania), nao waliivamia wizara hiyo kuwasilisha madai yao kuhusu mikopo na kuambiwa kuwa Serikali ingechukua hatua kuhusu madai hayo. Na siku tano zilizopita, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), waligoma na kuzua tafrani kubwa iliyosababisha uvunjifu wa amani na uharibifu wa mali, hatua iliyojibiwa na polisi ambao walivamia chuo hicho na kuwapiga wanafunzi kabla hawajaondoka na viongozi wa serikali ya wanafunzi na kuwasweka rumande. Wanafunzi hao walikuwa wanaishinikiza Serikali iwalipe fedha za mafunzo kwa vitendo na kutengeneza miundombinu chuoni hapo ambayo ilikuwa katika hali mbaya, licha ya madai yao mengine ya kuwapo uhaba mkubwa wa maji na wahadhiri. Lakini katika hatua ya kushangaza, Serikali ilisalimu amri ambapo waziri husika, Shukuru Kawambwa na mwenzake wa mambo ya ndani, Shamsi Vuai Nahodha, pamoja na kuamuru kuachiwa huru kwa viongozi wa wanafunzi waliokamatwa na polisi, walikodi ndege na kukutana na wanafunzi hao usiku kucha katika chuo hicho, na hatimaye kuwatangazia kuwa Serikali imekubali kutatua matatizo yao baada ya kuyaona kuwa ni ya msingi. Wakati Serikali ikihaha kutafuta suluhisho la matatizo ya Udom, jana wanafunzi wa Chuo cha Ardhi walianza rasmi mgomo wakiishinikiza Serikali itatue kero zao kumi, zikiwamo uhaba wa malazi kwa wanafunzi chuoni hapo na kushindwa kwa Serikali, kupitia bodi ya mikopo, kutangaza majina ya wanafunzi katika chuo hicho ambao watapewa mikopo. Uongozi wa chuo hicho unadai kuwa tayari umeipelekea bodi majina hayo wakati bodi hiyo inakana kupokea majina hayo. Hiyo ndio hali halisi katika vyuo vyetu vya elimu ya juu hivi sasa, na huo ndio utendaji usiowajibika wa Serikali na vyombo vyake vinavyohusika moja kwa moja na kuhudumia wanafunzi hao. Ni dhahiri kuwa wanafunzi wameishika pabaya Serikali ambayo inaonekana kuwa haina pa kutokea, kwani wamechoshwa na ngonjera za ‘ufinyu wa bajeti ya Serikali’ zinazoimbwa na vigogo wa serikali hiyo, huku wakiendelea kununua magari ya kifahari yenye gharama ya Sh280 milioni kila moja. Kama hali ndio hiyo, tutegemee migomo zaidi katika vyuo vingine, kwani wanafunzi katika vyuo hivyo nao watataka watekelezewe madai yao kama Serikali ilivyoahidi kufanya katika vyuo vilivyogoma. Lakini kama tulivyosema katika safu hii siku chache zilizopita, matatizo mengi katika vyuo vingi nchini yanatokana na kukatika kwa mawasiliano kati ya wanafunzi na uongozi wa vyuo, bodi ya mikopo na wizara husika.
|
No comments:
Post a Comment