Mbunge Chadema apigwa na polisi | Send to a friend |
|
UCHAGUZI wa Meya na Naibu wa Manispaa ya Arusha umechukua sura mpya baada ya kuibuka vurugu zilizosababisha Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, kukamatwa na Jeshi la Polisi na kupigwa hadi kupoteza fahamu na kulazwa katika Hospili ya mkoa huo Mount Meru. Vurugu hizo zilizodumu kwa takribani saa sita, zilisababisha askari wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia(FFU) kutumia mabomu ya machozi pamoja na maji ya kuwasha kuwatawanya maelfu ya wafuasi na wapenzi wa Chadema waliokuwa wamezingira ofisi za Manispaa hiyo na kufunga kwa muda Barabara ya Mkuu wa Mkoa na ya New Arusha Hotel. Vurugu hizo zilibuka baada Lema pamoja na madiwani wa Chadema kufika katika ofisi ya Manispaa hiyo, kupinga kufanyika kwa uchaguzi huo ambao uliitishwa na kinyemela bila kuwashirikisha madiwani wa chama hicho. Uchaguzi huo umedaiwa kufanyika kwa kuwashirikisha madiwani na wabunge wa CCM na wa TLP wawili ambao walimchagua Diwani wa Kata ya Olorien (CCM), Gaudence Lyimo, kuwa Meya na naibu Meya wake Michael Kivuyo ambaye ni Diwani wa Kata ya Sokoni kwa tiketi ya TLP. Kufuatia hali hiyo baadhi ya askari wa jeshi polisi waliokuwepo eneo hilo wakiwa wamevalia zana mbalimbali za kutuliza ghasia, walimzuia mbunge huyo kuingia ndani huku wakimwamuru atoke nje ya eneo hilo. Alipokataa askari hao walianza kumpa kipigo na kusababisha kupoteza fahamu kwa dakika saba kisha wakampakia katika gari lao hadi Kituo Kikuu cha Polisi mjini Arusha na kumweka rumande. Hali hiyo ilisababisha mamia ya wanachama na wafuasi wa chama hicho kujikusanya na kukizingira kituo hicho, huku wakiwatuhumu polisi kujiingiza katika masuala ya siasa ya kuisaidia CCM. Majira ya saa 9 Alasiri, mbunge huyo aliachiwa kwa dhamana na kurejea katika ofisi za Manispaa akiwa na kundi kubwa la wafuasi wa Chadema ambao walikuwa wakirusha maneno makali huku wengine wakitishia kuchoma moto ofisi ya manispaa. Katika ofizi hizo, FFU waliibuka tena na kurusha mabomu ya machozi pamoja na maji ya kuwasha, hali iliyosabisha Lema ambaye alikuwa akizungumza na madiwani wa Chadema kukimbia kisha kuanguka na kupoteza fahamu kwa dakika kama tano na kukimbizwa katika Hopitali ya Mount Meru kwa matibabu zaidi. Mwananchi Jumapili ilishuhudia jana jioni Lema akiwa amelazwa katika moja ya wodi katika hospitali ya Mount Meru akiwa na mkewe. Wakati Lema akiwa amelazwa katika wodi hiyo umati mkubwa wa wafuasi wa Chadema ulikuwa umetanda nje ya hospitali hiyo wakisubiri kujua hatima ya afya ya mbunge wao. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Tobias Adengenye alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba kukamatwa kwake kunatokana na Lema kukaidi amri ya polisi. Awali Lema aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa kipigo alichopata, kilimsababisha matatizo ya mbavu pamoja na mkono wa kulia kuumia. “Pamoja na mambo mengine, nina maumivu makali sana katika sehemu za mbavu pamoja na mkono wa kulia,” alisema Lema. Kiongozi wa kambi ya upinzani Arusha ambaye ni Diwani wa Chadema, Kata ya Elerai, John Bayo, aliwaambia waandishi wa habari kuwa wanatarajia kwenda mahakamani kesho (Desemba 20) kufunuga kesi kupinga uchaguzi huo kutokana na baadhi ya kanuni kutofuatwa. Bayo alifafanua kwamba mojawapo ya kanuni iliyokiukwa ni kutozingatiwa kwa idadi ya theluthi mbili ambao ni madiwani 20 wenye mamlaka ya kumchagua meya na naibu wake. Katika Manispaa hiyo, CCM ina jumla ya madiwani 14 huku Chadema ikiwa na jumla ya madiwani 16 huku TLP ikiwa na wawili. “Jumatatu (kesho), tunaenda mahakamani kupinga uchaguzi huo, kwanza hatukupewa barua ya kuhudhuria uchaguzi leo baada ya jana kuhairishwa, lakini pili idadi yao haikutimia kumchagua meya na naibu wake kwani sheria inasema ni theluthi mbili itakamilisha uchaguzi, wao walikuwa 15,” alisema Bayo. Hata hivyo, uteuzi Diwani wa TLP wa Naibu Meya umezua utata kwa vile awali alikuwa akiwaunga mkono Chadema na kwamba hadi saa 5 asubuhi alikuwa katika mkutano wa madiwani wa upinzani. “Alituaga kuwa anakwenda ndani ya ofisi za Manispaa kujua nini hatma ya uchaguzi, lakini hakurudi hadi tulipopata taarifa kuwa amechaguliwa kuwa Naibu meya,’’ kilisema chanzo chetu. Alipoulizwa kuhusiana na hali hiyo, Katibu wa Itikani na Uenezi wa CCM, John Chiligati alisema: “Uchaguzi si wa kinyemela unajulikana nchi nzima, lakini siwezi kuzungumza lolote kwa sasa kwa kuwa bado sijapata taarifa rasmi kuhusu hali hiyo”. Uchaguzi huo ulikuwa ufanyike juzi, lakini uliahirishwa na Msimamizi wa Uchaguzi, Estomi Chang'a ambaye pia ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Arusha kufuatia kutokea malumbano baada ya madiwani wa Chadema kupinga kitendo cha CCM kumteua, Mary Chatanda ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu mkoani Tanga na Katibu wa CCM mkoani Arusha kuwania nafasi hiyo ya umeya. Sababu nyingine ni kambi ya upinzani kupinga kitendo cha msimamizi wa uchaguzi kumzuia Diwani wa viti maalumu wa TLP, Mwamvua Wahanza kutopiga kura kwa madai ya kutothibitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec). Katika hatua nyingine, askari waliokuwa wakilinda ofoso manispaa hiyo waliwazuia baadhi ya waandishi wa habari kuingia ndani kwa madai kuwa hawana mwaliko rasmi huku isipokuwa mwandishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Leornad Manga. Pamoja na waandishi kuwasomea kanuni za kudumu za mikutano na shughuli za manispaa, walikataliwa kuingia. Juhudi za kumpata Mkurugenzi wa Manispaa ya Arusha, Chang'a kuzungumzia suala hilo zilishindikana kutokana na simu yake ya mkononi kushindwa kupokelewa hadi tunakwenda mtamboni. Alipoulizwa kuhusu hali hiyo, Mwasisi wa Chadema, Edwin Mtei aliiambi Mwananchi Jumapili jana kuwa analaani sana kitendo hicho cha kukamatwa mbunge wao na kwamba kinaonyesha wazi kuwa CCM bado imechaganyikiwa kutokana na kupoteza majimbo mengi katika uchaguzi mkuu. Jambo la kushangaza uchaguzi wa mameya umekuwa na matatizo makubwa katika maeneo yote ambayo upinzani una madiwani wengi huku wakurugenzi wa halmashauri hizo, ambao ndiyo wasimamizi kwaikidaiwa kuhusika kupanga njama za kukipendelea Chama Cha Mapinduzi kwa kukiuka taratibu. Halmashauri za Manispaa zilizokumbwa na tatizo hilo na kusababishwa uchaguzi kuahirishwa juzi ni Arusha, Mwanza, Tanga na Kigoma ambzi zite CCM ina madiwani wachache. Hata hivyo, uchaguzi kwenye halmashauri ambazo CCM haina upinzani ulifanyika bila matatizo zikiwemo manispaa za Mkoa wa Dar es salaam. Wakati huo huo matokeo ya mameya wa halmashauri nchini yanaendelea kutangazwa katika baada ya kumalizika kwa uchaguzi katika mikoa yote. Suzy Butondo kutoka Shinyanga anaripoti kuwa, Gulam Hafidh alichaguliwa kuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga na Naibu wake ni Agnes Machiya, huku Nyakafuru Mathias Nyororo akichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Bukombe na Makamu wake ni Busiga Vicent Mwamalasa na Justine Sheka amekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu na Makamu wake ni Samson Shimbi. Katika Halmashauri ya Kahama, Mwenyekiti ni Ntobo Nkwabi na Makamu ni Chela Mbako Mabubu na Wilayani ya Maswa, mwenyekiti ni Stephen Dwese akisadiwa na Ndila Mayeka. Meatu Mwenyekiti ni Ng’hoboko Pius Machungwa na Makamu ni Mwandoya Basu Kayungilo. Mwenyekiti Shinyanga Vijijni ni Amos Mshandete ma Makamu wake ni Solwa George Lunyembeleka. Naye Hussein Semdoe, anaripoti kutoka Tanga kuwa, Jaila Mussa Semdoe alipita bila kupingwa kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri Wilaya ya Kilindi na Abdallah Ndalo kuwa Makamu. Naye Christopher Maregesi, anaripoti kutoka Bunda kuwa, Joseph Marimbe alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo na Sospeter Masambu, kuwa Makamu Mwenyekiti. |
No comments:
Post a Comment