Friday, October 8, 2010

KUELEKEA MECHI YA KESHO JUMAMOSI NA TAIFA STARZ, MOROCCO WAJA NA KILAKITU, KUANZIA MAJI NA VYAKULA VYAO KWA KUOGOPA KUFANYIWA HUJUMA...


Wachezaji wa Morocco wakifanya mazoezi kwenye uwanja wa Taifa nchini Tanzania



KOCHA wa timu ya Taifa ya Tanzania, Jan Poulsen amesema hawezi kuingiza timu uwanjani ikiwa na mawazo ya kushinda pekee bali wataingia uwanjani wakiwa na lengo na njia ya kutafuta matokeo mazuri.

Akizungumza na katika mahojiano maalum jana katika Hoteli ya Atrium ya jijini Dar es Salaam alisema atakachokifanya katika mechi ya Jumamosi dhidi ya Morocco ni kuingiza timu uwanjani ikiwa na mawazo ya kutafuta njia ya kupata ushindi na si kufikiria ushindi katika mechi hiyo.

"Hatuwezi kufikiria ushindi badala yake tunafikiria njia na mbinu zitakazotuwezesha kupata matokeo mazuri ikiwa ni pamoja na ushindi, "alisema Poulsen na kuongeza:

"Timu ikiingia uwanjani ikiwa na mawazo ya kupata ushindi inajiweka katika mazingira magumu ya kufanya vizuri hasa pale inapotokea kwamba wapinzani wenu wamekuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza."

Mdenmark huyo alisema kulingana na aina ya wachezaji alionao analazimika kufikiria njia zinazoweza kumpatia matokeo mazuri ili aendelee kujiweka katika mazingira mazuri zaidi ya kufuzu kucheza fainali hizo.

"Ninatambua kuwa Morocco ni timu nzuri iliyoundwa na wachezaji wengi wanaocheza ligi kubwa barani Ulaya, pia katika orodha ya ubora wa soka Afrika wako juu zaidi ya Tanzania, lakini hiyo haiwezi kuwa kigezo cha kushindwa kupata matokeo mazuri katika mechi hiyo,"alisema Poulsen.

Katika hatua nyingine kocha huyo alisema amewaandaa wachezaji wake vizuri kisaikolojia ili waweze kufanya vizuri katika mechi hiyo na kikubwa alichowaeleza ni kutokuangalia wachezaji wenye majina makubwa.

Wakati Poulsen akisema hayo, wapinzani wake timu ya taifa ya Morocco ‘Atlas Lions’ wamewasili juzi usiku kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere huku wakikataliwa kupitia kwenye eneo la watu mashuhuri, VIP licha ya balozi wao mdogo hapa nchini kulazimisha wapitie hapo.

Timu hiyo iliwasili juzi saa 4:38 usiku ikiwa na kundi la watu 40 tayari kwa mchezo wa kesho dhidi ya Taifa Stars kwenye Uwanja wa Taifa, ikiwa ni mfululizo wa michuano ya kuwania kufuzu kucheza Fainali za Afrika zitakazoandaliwa kwa pamoja kati ya Guinea ya Ikweta na Gabon.

Mmoja wa maofisa usalama uwanjani hapo alisema kuwa licha ya balozi mdogo kufika uwanjani hapo, alikataliwa agizo lake kuwa timu hiyo ingepitia kwenye eneo hilo la VIP ambalo kimsingi haliruhusu kundi kubwa zaidi ya watu watatu hadi watano na wenye umashuhuri mkubwa.

"Haiwezekani, kwanza wale hawana sifa za kupitia VIP, balozi anataka kulazimisha tu kupita eneo lile, na pia hawakutakiwa kuletewa basi ndani, hawa si watu maalum," alilalamika mmoja wa maofisa hao wa usalama uwanjani hapo.

Hata hivyo, walikubaliwa kuingiza ndani basi lao walilokodi na wachezaji waliingia haraka bila kufuata ukaguzi wa Idara ya Uhamiaji.

Habari zilizopatikana juzi usiku uwanjani hapo, ni kwamba wachezaji hao waliingia bila kukaguliwa na wakati maofisa wa uhamiaji pamoja na msemaji wa TFF, Florian Kaijage wakihaha kutaka taratibu za ukaguzi zifanyike, wachezaji hao walipitishwa mlango wa nyuma na kupanda basi huku wakitoka kwa mafungu na kuondoka wakiwa chini ya ulinzi mkali kwenda hotelini.

Mmoja wa mawakala wa wachezaji hao waliokuwa wakizungumza Kiarabu na Kifaransa, alisikika akisema kuwa wachezaji hawakukaguliwa, lakini viongozi walioandamana na timu walikuwa ndani kukamilisha taratibu za uhamiaji.

Msimamizi mkuu wa msafara huo wa Jeshi la polisi, Kamishna Msaidizi, Marijaney Msata aliwaambia waandishi wa habari kushangazwa na usiri unaofanywa na maofisa wa timu ya Morocco ikiwa ni pamoja na kupangua taratibu za usafiri ambao ilikuwa watoke kwa msafara kwenda hotelini.

Mapema waandishi wa habari walipotaka kuzungumza na makocha akiwemo kocha wa muda wa timu hiyo, Dominique Cuperly , walizuiwa na watu ambao hata hivyo hawakufahamika mara moja na inawezekana hata wachezaji hawakutakiwa kuzungumza na mtu yeyote na ilikuwa hivyo.

Habari ambazo Mwananchi ilizipata uwanjani hapo zinasema Morocco hawakutaka TFF kujihusisha na chochote na wametumia sh9milioni kukodi magari ya Kampuni ya Lion of Tanzania kuanzia basi la wachezaji, magari ya maofisa wao na waandishi wao wa habari kwa siku tatu.

Kazi ilikuwa katika gari aina ya canter lenye namba T475AKK ambalo baada ya kupakiza mabegi ya vyakula, maji na vyombo vya kuhifadhia vyakula 'hotpots' kubwa, hawakutaka hata Mtanzania kuvigusa na kulikuwa na watu maalum waliokuwa wakilinda kuanzia Uwanja wa Ndege hadi kwenye Hoteli ya Kempinski walikofikia.

Mjumbe wa TFF, Idd Mshangama aliyeiwakilisha taasisi hiyo, alikiri kuwepo hali hiyo na kusema kama wao (Morocco) wamefanya hivyo, TFF wajipange kujitegemea kwa kila kitu watakapofika Rabat kwa mchezo wa marudiano. Mwenyekiti wa Makocha, Ramadhani Mambosasa naye alikuwa mmoja wa waliokuja kuilaki timu hiyo.

Wachezaji wa timu hiyo, leo watakuwa kwenye Uwanja wa Taifa kufanya mazoezi ya mwisho ikiwa ni siku moja kabla ya mechi hiyo ambayo Taifa Stars inatakiwa kushinda na kuweka hai matumaini ya kucheza Fainali za Afrika 2012. Katika mchezo wa kwanza, Stars ilitoka sare ya 1-1 na Algeria mjini Algiers.

Wakati huo huo, CECAFA imezitakia kila la kheri timu zake isipokuwa Kenya na Uganda ambazo zinakutana mjini Nairobi. Mechi za timu hizo ni kati ya Tanzania na Morocco wakati Ethiopia inacheza na Congo DR huku Sudan ikionyeshana na Ghana.

No comments:

Website counter