Wednesday, October 6, 2010

AMA KWELI SIASA SIO MCHEZO, SIKIA HII KALI...

Dk Slaa ampigia debe Dk Mwakyembe Send to a friend


Dk Harrison Mwakyembe


MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chadema, Dk Willibrod Slaa jana hakusita kuonyesha hisia zake kwa mgombea ubunge wa Jimbo la Kyela kwa tiketi ya CCM, Dk Harrison Mwakyembe alipowataka wananchi kumchagua aendelee kuwawakilisha.Dk Slaa, ambaye pamoja na Mwakyembe walijulikana kama vinara wa upambanaji dhidi ya ufisadi katika Bunge la Tisa, alisema hayo hali akijua kuwa Chadema ina mgombea kwenye jimbo hilo anayeitwa Eddo Mwamalala.

Lakini uamuzi wake wa kumpigia debe Dk Mwakyembe uliambatana na masharti matatu, moja likiwa gumu kutekelezwa na mteule huyo wa CCM katika mkakati wake wa kurejea kwenye chombo hicho cha kutunga sheria.

"Sharti la kwanza, Dk Mwakyembe atatakiwa kutompigia kampeni (mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya) Kikwete," alisema Dk Slaa kwenye mkutano uliofanyika Uwanja wa Mwakangale na kuhudhuriwa na watu wengi kiasi.

“Dk Mwakyembe ni rafiki yangu wa damu, kama kweli unautaka ubunge wa hapa, lazima asimpigie kampeni mgombea urais wa CCM na badala yake uninadi mimi ili niweze kuikomboa nchi hii.”

Mbunge huyo wa zamani wa Karatu alitaja sharti la pili kuwa ni kuweka maslahi ya wananchi mbele badala ya kuweka mbele maslahi ya CCM.
Dk Slaa alitaja sharti la tatu kuwa ni Mwakyembe kuacha kile alichokiita unafiki wa CCM wa kujigamba kwamba chama hicho kimefanya mambo mengi wakati hakuna lolote.

Chadema imesimamisha mgombea Mwamalala, lakini inaonekana wananchi wengi wa Kyela bado wanamtaka Dk Mwakyembe aendelee.

“Huu ni mkataba tumewekeana leo, kama Dk Mwakyembe anautaka ubunge asikiuke kwani akifanya hivyo tu, mpigieni kura mgombea wa Chadema,” alisema Dk Slaa ambaye alisema hana ugomvi na Dk Mwakyembe.

Dk Slaa alisema ameshangazwa na mgombea ubunge wa Chadema kumpigia kampeni Dk Mwakyembe katika mkutano mmoja ulifanyika jana kwenye Kijiji cha Ipalula.

“Nimemsimamisha mgombea wangu pale Ipalula, lakini badala ya kujinadi, akamnadi Dk Mwakyembe. Najua anakubalika ila akirudia nitampiga viboko,” alisema Dk Slaa.

Dk Mwakyembe aliibuka kuwa mmoja wa wabunge wachache waliolitia joto Bunge la Tisa kutokana na uwezo wake wa kujenga hoja, na umaarufu wake ulipaa wakati alipoiongoza Kamati Teule ya Bunge kuchunguza kashfa ya utoaji zabuni ya ufuaji umeme wa dharura kwa kampuni tata ya Richmond Development LLC.

Ripoti ya kamati yake ilisababisha Edward Lowassa kujiuzulu wadhifa wake wa Waziri Mkuu na kufuatiwa na mawaziri wawili waliowahi kushika Wizara ya Nishati na Madini, Nazir Karamagi na Ibrahim Msabaha.

Kashfa hiyo pamoja na ile ya wizi wa fedha kutoka kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ndizo zilizotawala mikutano mingi ya Bunge la Tisa kutokana na wabunge kuhoji utekelezwaji wa maazimio 23 ambayo serikali ilitakiwa iyatekeleze.

Naye Mwamalala aliwaambia wananchi kwenye mkutano huo kuwa kama wananchi bado wanampenda Dk Mwakyembe, wampe kipindi cha pili na kwamba zamu yake itakuwa mwaka 2015.

“Mimi sioni haja ya kugombanishwa wenyewe kwa wenyewe. Pimeni kwa umakini na muamue, ila kama mkiona mie bado kidogo, nipumzisheni hadi 2015,” alisema Mwamalala akiongeza kuwa wote wanagombania kusimamia ilani za vyama vyao.

Akiwa kwenye mkutano uliofanyika Inyala, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Dk Slaa alimkebehi Kikwete kwa kutaka Watanzania wamkumbuke kwa vigezo ambavyo havijawasaidia kitu maishani mwao.

Alisema awaachie wananchi wamkumbuke kwa yale aliyofanya na badala ya kujinadi wakati anajua hajafanya kitu cha kusababisha akumbukwe.

“Hivi ukitaka ukumbukwe, lazima useme umefanya nini au hiyo ni kazi ya wananchi kuamua wakukumbuke,” alihoji Dk Slaa na kuongeza kuwa yeye hataki kukumbukwa kwa kuwambia wananchi amefanya nini ila wao wapime nini kafanya na wamuenzi kwa hayo.

Alitolea mfano wa Baba wa Taifa, Marehemu Julius Kambarage Nyerere ambaye aliliongoza taifa kwa zaidi ya miaka 20 na wananchi wanamkumbuka kwa kumjengea nyumba bila yeye kuwaomba.

“Hivi Nyerere alijitangaza kafanya nini ili akumbukwe? Mbona hata mtoto aliyezaliwa leo anamjua kwa mazuri aliyofanya, kwa nini uwaombe wakukumbuke wakati hujawafanyia mambo mazuri ya kukufanya ukumbukwe,” aliuliza Dk Slaa.

Dk Slaa amesema Kikwete ataingia kwenye historia kwa kukumbukwa na Watanzania kwa kushindwa kujibu swali kuwa 'kwa nini nchi yako maskini wakati ina rasimali nyingi'. Alisema swali hilo aliulizwa katika msafara wake mmoja nje ya nchi.

Aliongeza kuwa atakumbukwa kwa kusema msongamano wa magari uliopo jijini Dar es salaam ni ishara ya maendeleo makubwa bila ya kutafuta njia muafaka wa kutatua tatizo hilo.

“Hivi kama gari la rais linawekewa mafuta yaliyochakachuliwa, hali ikoje kwa wanachi wa kawaida? Ataka wananchi wasahau haya na kukumbukwa kwa barabara, vituo vya afya na shule zisizo na walimu,” aliuliza Dk Slaa huku akishangiliwa na umati wa wananchi.

2 comments:

Anonymous said...

Отличная статья! большое спасибо автору за интересный материал. Удачи в развитии!!!
http://www.miriadafilms.ru/
kinyaiyas.blogspot.com

Anonymous said...

Почему регистрация не работает ?

Website counter